UGONJWA WA POLIO NA UMUHIMU WA KUMPATIA MTOTO CHANJO YA UGONJWA HUU


Polio ni ugonjwa wa kuambukiza unaosababishwa na virusi vinavyoingia mwilini kupitia mdomoni kwa njia ya kula chakula au kunywa kinywaji. 

Virusi hivyo hupatikana kwenye kinyesi cha binadamu ambacho huwa na virusi vya ugonjwa wa polio ambapo kinyesi hicho kikiingia kwenye maji na yakatumiwa na mtu kwa njia ya kupikia chakula au kunywa huweza kuambukizwa ugonjwa huo. Takriban asilimia 90 hadi 95 ya wanaoambukizwa ugonjwa huu huwa hawaoneshi dalili zozote, huku asilimia 5 hadi 10 ya watu huonesha dalili hafifu za homa, maumivu ya kichwa, kutapika, kuharisha, mishipa ya shingo kukaza na maumivu katika miguu na mikono. 

Hali hiyo hutokana na virusi hivyo vinapofika kwenye tumbo huweza kusafiri hadi kwenye ubongo na uti wa mgongo ambapo mgonjwa huweza kuhisi maumivu ya kichwa, kukakamaa kwa shingo pamoja na maumivu ya miguu na mikono. Kwa kawaida watu hawa hurejea katika hali ya kawaida baada ya wiki moja au mbili. 

Asilimia 0.5 ya waathrika huweza kupata udhaifu wa misuli suala linalosababisha kushindwa kutembea. Hali hiyo huweza kutokea katika masaa kadhaa baada ya maambukizo. Virusi vya polio vinapofika tumboni huweza kuzaliana na kuongezeka, hivyo kuanza kushambulia neva na kusababisha mgonjwa kupooza baadhi ya viungo.

 Ugonjwa huu, huwapata zaidi watoto walio chini ya umri wa miaka miwili kuliko wale ambao wameshavuka umri huo. Ingawa ni asilimia ndogo sana ya wanaopatwa na polio huweza kupata ulemavu wa mwili wa kudumu, lakini hatari hiyo inalazimu ugonjwa huo kupewa umuhimu mkubwa na kuzuiwa kupitia chanjo. 

Ugonjwa wa polio unaweza kuzuilika kupitia chanjo, hata hivyo dozi kadhaa hutakiwa ili chanjo iweze kuwa na athari. Pale mtu anapopatwa na ugonjwa huu huwa hakuna dawa maalumu ya kumtibu. Mwaka 2013 polio iliwaathiri watu 416 duniani ikilinganishwa na mwaka 1988 ambapo watu laki na nusu walipatwa na ugonjwa huu. Mafanikio hayo yametokana na kupewa umuhimu chanjo kwa watoto takribani katika maeneo yote duniani suala lililoleta matumaini ya kutokomezwa ugonjwa huo ifikapo mwaka 2018. Lakini mwaka huu wa 2017 ugonjwa wa polio ulishuhudiwa katika nchi za Afghanistan, na Pakistan.

DALILI ZA UGONJWA HUU

Mtu mwenye ugonjwa huo hupata dalili za kuumwa na kichwa, shingo kukakamaa mwili na miguu na mikono kuwa na maumivu. Zipo dalili nyingine ambazo hazionekani mara kwa mara ambazo kupelekea baadhi ya viungo kulegea au kupooza. Ugonjwa huu unaweza kuathiri sehemu mbalimbali za mwili ikiwemo mikono, miguu na sehemu nyinginezo. Aidha baadhi ya watu wanaweza kuathirika kuanzia maeneo ya nyonga kushuka chini jambo linalopelekea kukosa mawasiliano kati ya sehemu hizo mbili hata kupelekea kushindwa kudhibiti haja kubwa na ndogo. Zile sehemu zinazokuwa zimeathirika zinaweza kupata nafuu pale mgonjwa atakapokuwa anafanya mazoezi ya viungo kwa kiasi kinachotakiwa.


Image result for poliomyelitis
Kinga na matibabu yake


Ugonjwa wa polio kwa bahati nzuri unaweza kuzuilika kwa kupata chanjo hasa kwa watoto wadogo chini ya miaka miwili. Chanjo ndio njia pekee ya kupambana na ugonjwa huu ambao una madhara hasa ya kusababisha ulemavu na hata kumfanya mtu awe tegemezi maishani. Chanjo hizo huweza kutolewa kwa watoto kuanzia miezi miwili ambapo hupewa dawa kwa njia ya matone na sindano. Hata hivyo watoto na watu wazima waliopata chanjo ya kuzuia polio wanaweza kupata ugonjwa huo tena ingawa unakuwa hauna makali sana ukilinganisha na yule ambaye hajapata chanjo hiyo. Aidha kwa wale ambao wamepatwa na ugonjwa huu hakuna dawa ya kuweza kutibu ugonjwa huo zaidi ya matibabu kwa njia ya mazoezi. Kwa kawaida ni vigumu kutibu mtu aliyepooza zaidi ya kumpatia dawa ya kupunguza maumivu kwani hakuna dawa itakayoweza kuondoa kupooza. Kutokana na ugonjwa huu kukosa tiba chanjo, watu wanatakiwa kuchukua tahathari kubwa hasa wale wenye kuwahudumia wagonjwa wa polio.
 
Image result for polio
Watu wanaowahudumia wagonjwa wa polio wanatakiwa kuzingatia zaidi usafi pale wanapomaliza kuwahudumia wagonjwa hao kwani wanaweza kujisahau na kula kitu jambo linaloweza kuwapatia maambukizi ya ugonjwa huo. Pia ni muhimu wazazi na walezi kuhakikisha mtoto amepata matone akiwa na umri wa miezi miwili, mitatu na minne. Pia hata wale ambao waliwahi kuugua ugonjwa huo na kupona, wanaweza kuugua tena kwa mara ya pili ingawa sio wote. Inashauriwa kuwa mtoto au mtu mzima aliyepata ugonjwa huo na kupooza ale chakula bora pamoja na kufanya mazoezi ili kuipa nguvu misuli iliyobaki mwilini bila kuathirika. Katika mazoezi hayo anatakiwa kufuata ushauri wa daktari ili kuweza kufanya mazoezi kadiri inavyotakiwa kwani iwapo atazidisha mazoezi anaweza pia kupata madhara. 

Kama amepata matatizo kwenye miguu anatakiwa kusaidiwa kutembea kadri anavyoweza na baada ya muda apatiwe msaada wa kutembea kama vile kutafutiwa magongo ya kutembelea. Aidha kwa watu waliowahi kuugua ugonjwa huo wanaweza kuwa na matatizo ya kupumua yanayosababishwa na ugonjwa huo kudhohofisha misuli ya kupumua hivyo wanaposhindwa kupumua wanatakiwa kusaidiwa kupumua kwa njia yoyote ikiwemo ya kuwaweka kwenye mashine za kupumulia.


Mwisho niitimishe kwa kubainisha maswali ambayo huulizwa mara kwa mara kuhusiana na ugonjwa wa Polio. Miongoni mwa maswali hayo ni kama vile,

 siwezi kukumbuka ikiwa watoto wangu walipata viwango vyote 4 vya chanjo wakati walipokuwa wachanga, je wanahitaji kupatiwa chanjo tena? 

Jibu ni ndiyo, ikiwa hauna uhakika kama watoto wako walipata viwango vyote vinne vya chanjo ya ugonjwa wa kupooza wa polio walipokuwa wachanga, unashauriwa kuwapatia chanjo tena. Viwango vinne hutoa kinga kwa asilimia 100 dhidi ya ugonjwa huu. Hii ina maana ya kwamba ikiwa ulipata viwango vyote 4 vya chanjo ya kupooza, basi umelindwa dhidi ya ambukizo la ugonjwa wa polio katika maisha yako. Kwa hivyo ni muhimu kwa kila mtu katika jamii kupata chanjo dhidi ya polio na kuhakikisha ya kwamba kila mtu anapata viwango vyote 4 vya chanjo hiyo.

 Swali jingine ni kwamba, je, ikiwa watoto wangu watapewa chanjo wanaweza kuwa wagonjwa na hatimaye kufa? 
Tunaweza kusema kuwa, huu ni wasiwasi wa kawaida kwa wazazi wakati wanapotakiwa wawape watoto wao chanjo dhidi ya kupooza. Na jibu ni la hasha, chonjo ya polio ni kwa ajili ya kumlinda mwanao asipatwe na ulemavu na wala sio kumletea madhara au kifo. Ni muhimu kujua kuwa, polio ni ugonjwa unaosababishwa na kirusi na wala hauwezi kutibiwa pindi mtu anapoambukizwa. Hata ikiwa mtu hana dalili za maambukizo, bado anaweza kuambukiza watu wengine, hasa mahali ambapo hakuna usafi na udhibiti bora wa afya. Ingawa katika kesi nyingi, mtu aliyeambukizwa huwa hana dalili zozote, kuna visa ambavyo mtoto au mtu mzima hupooza kutokana na maambukizo ya Polio. Tukumbuke kuwa ugonjwa wa polio ni chanzo muhimu cha kupooza, ugonjwa ambao tunaweza kujikinga nao na kuwakinga wengine kupitia chanjo na kudumisha usafi. Kwa hivyo ni muhimu kwa watoto wote na watu wazima duniani kote kupata chanjo dhidi ya polio.
 

Na swali la mwisho ni kuwa, je, ninahitaji kumpeleka mtoto aliye na zaidi ya miaka 3, apate chanjo wakati wa kampeini za chanjo? Jibu pia ni ndiyo, ni muhimu kwa watoto wote kushiriki katika chanjo wakati wa kampeni za chanjo za jumla. Polio ni ugonjwa ambao unaweza kuwaathiri watoto wa umri wowote na watu wazima pia. Ni muhimu kila mtu achanjwe dhidi ya ugonjwa huu. Katika maeneo ambapo udhibiti wa afya ni mbovu, kuna ukosefu wa maji safi na usafi hauzingatiwi, ugonjwa huu huenea kwa urahisi katika jamii. Chanjo dhidi ya polio ndiyo njia pekee na mwafaka ya kupambana na ugonjwa huu na ni lazima sote tuunge mkono juhudi za kutokomeza polio duniani!





 

No comments