Mzio au aleji (allergy) ni matokeo ya mpambano uliopitiliza kati ya kinga ya mwili na kitu chochote (ambacho kwa ujumla huwa hakina madhara kwa mwili) inapotokea kimeingia ndani ya mwili au kimegusa sehemu fulani ya mwili.
Aleji husababishwa na nini?
Kuwa na mzio ni jambo la kawaida. Haishangazi basi kuona kuna
baadhi ya watu wanakuwa na mafua karibu kila siku au wengine wanashindwa kuvaa
baadhi ya vitu kama saa au cheni za dhahabu kwa vile tu huvimba mwili au
kuwashwa pindi wanapofanya hivyo.
Kwa kawaida kinga ya mwili huulinda mwili dhidi ya vitu
mbalimbali hatari kwa afya kama vile vimelea vya bakteria na virusi, lakini
wakati mwingine inaweza kupambana pia na vitu ambavyo havina madhara yeyote kwa
mwili (ambavyo huitwa allergens). Watu wenye aleji/mzio huwa na hisia zisizo za
kawaida za mwili dhidi ya baadhi ya vitu.
Mwili unapokumbana na vitu vinavyosababishia aleji (yaani
allergens), mfumo wa kinga ya mwili huzalisha kemikali mbalimbali ikiwemo
histamine ambayo hupambana na allergens hizo. Mpambano huu ndo husababisha mtu
kuwa na dalili za aleji/mzio.
Matatizo ya kinasaba pamoja na hali tofauti tofauti za
kimazingira zote zinahusika sana katika kusababisha mtu kuwa na mzio. Baadhi ya
vitu vinavyosababisha mzio (allergens) ni pamoja na vumbi vumbi, baadhi ya
dawa, baadhi ya vyakula, kung'atwa na wadudu kama vile nyuki, aina fulani ya
uyoga, vumbi vumbi la maua (pollens) n.k.Wapo baadhi ya watu ambao
hukumbana na mzio pindi wanapokuwa katika mazingira ya joto au baridi wakati
wengine hupatwa na mzio pindi wanapopigwa na jua kali. Wakati mwingine, hata
msuguano kidogo tu wa ngozi unaweza kuwasababishia baadhi ya watu dalili fulani
fulani za mzio.
Kama nina aleji mtoto wangu pia
anaweza kupata aleji hiyo hiyo?
Kwa kawaida, mzio wa aina fulani huwa haurithishwi miongoni mwa
wanafamilia. Kwa mfano kama mzazi ana aleji na baridi si lazima watoto wake pia
wawe na aleji hiyo hiyo ya baridi ingawa wanaweza kuwa na aina nyingine ya
aleji. Uwezekano wa mtoto kupata aleji huongezeka zaidi iwapo wazazi wote
wawili wana aleji na vitu fulani fulani na huwa mkubwa zaidi iwapo mama ndiye
mwenye aleji.
Nini dalili za mtu mwenye aleji?
Dalili za aleji zipo nyingi kutegemeana na eneo gani la mwili
linahusika, lakini kwa ujumla
- Kama ni mfumo wa hewa ndiyo
ulioguswa, mtu anaweza kuwa na matatizo katika kupumua (kikohozi au
kubanwa na pumzi, makamasi na kuziba kwa pua, muwasho kwenye pua na koo,
au kupumua kwa kutoa sauti kama mtu anayepiga filimbi)
- Kama macho yataguswa, muhusika
hujihisi hali ya kuchoma choma, kutiririkwa na machozi na muwasho kwenye
macho, macho kuvimba na kuwa mekundu
- Iwapo mtu atakula kitu ambacho ana
aleji nacho anaweza kuwa na dalili kama vile kuharisha, kichefuchefu,
kutapika, Kusokotwa au kuumwa na tumbo au hata hali mbaya ya kutishia
maisha.
- Allergens zinazogusa ngozi zinaweza
kusababisha ngozi kuwa na mabaka mabaka, kubabuka, kuvimba, muwasho, kuota
vipele na malengelenge, michubuko au ngozi kuwa nyekundu.
- Aleji zinazohusisha mwili mzima
zinaweza kuwa na mkusanyiko wa dalili zote za hapo juu
Wakati mwingine aleji inaweza kuzorotesha hali ya baadhi ya watu
wenye magonjwa kama ugonjwa wa ngozi wa eczema au pumu kufanya iwe mbaya zaidi.
Vipimo na uchunguzi
Mgonjwa ataulizwa kuhusu historia ya tatizo lake, ni lini
lilianza na vitu gani humfanya awe hivyo. Aidha tabibu pia atapenda kufahamu
kuhusu dalili nyingine zinazoambatana na tatizo linamlomkabili mgonjwa.
Baadaye vipimo vya aleji vinaweza kufanyika ili kufahamu hasa ni
kitu gani mgonjwa ana aleji nacho na kama kweli dalili alizo nazo mgonjwa ni
kweli zinatokana na aleji au zinatokana na sababu nyingine. Hii ni kwa sababu
kuna baadhi ya mambo yanaweza kumsababishia mtu kupatwa na dalili zinazofanana
kabisa na mtu aliye na aleji ya kitu fulani.
Kwa mfano matumizi ya aina fulani ya dawa zinaweza kumsababishia
mtu kupata mikwaruzo au michubuko katika ngozi inayofanana na aleji nyingine,
au mtu anaweza kuwa na mafua au kikohozi kwa sababu ya maambukizi ya bakteria
au virusi na si kwa vile inatokana na aleji.
Kipimo maarufu kabisa cha kutambua aleji kwa mtu ni kipimo cha
ngozi (skin testing) ambapo mgonjwa huwekewa baadhi ya vitu
vinavyohisiwa kumletea aleji juu ya ngozi yake na kisha ngozi huchomwa kidogo
kwa sindano ili hivyo vitu viweze kuingia ndani ya ngozi wakati huo daktari
akichunguza kama kuna mabadiliko yeyote (kama vile uvimbe au ngozi kuwa
nyekundu) katika eneo lilichomwa. Kipimo cha namna hii hufaa zaidi kwa watoto
wadogo kwa vile ni rahisi kufanyika kwao bila usumbufu mkubwa sana.
Aina nyingine yay kipimo cha aleji cha ngozi hufanyika kwa kubandika
vitu vinavyohisiwa kuleta aleji kwenye ngozi (patch testing) au kuchoma sindano
zenye allergens sehemu ya juu ya ngozi (intradermal injection) na kuchunguza
uwepo wa mabadiliko yeyote katika ngozi.
Vipimo vingine ni pamoja na vipimo vya damu huonesha ongezeko la
immunoglobulin E ambayo huashiria uwepo wa vitu vinavyosababisha aleji, na
kipimo cha Full Blood Picture chenye kuonesha ongezeko la eosinophil (ambayo ni
sehemu mojawapo ya chembe nyeupe za damu) iwapo kuna aleji.
Lakini pia daktari anaweza kukushauri kuepuka baadhi ya vitu
hasa dawa au aina fulani za vyakula ili kuona kama utapata nafuu yeyote au
kukushauri kutumia baadhi ya vitu anavyohisi vinakuletea matatizo ili kuona
kama utapata dalili zozote zile.
Ni kweli Aleji inatibika?
Njia bora kabisa ya kutibu na kupunguza uwezekano wa kupata
aleji ni kutambua kitu au vitu vinavyokusababishia hali hiyo na kuviepuka. Kama
ni chakula au dawa au kemikali, epuka kabisa matumizi yake, na kama ni vumbi
jitahidi kukaa nalo mbali. Kadhalika shambuli kali la aleji laweza kusababisha
muhusika kulazwa hospitali kwa vile lisipothibitiwa kifo kinaweza kutokea.
Zipo aina mbalimbali za dawa zitumikazo kutibu na kuzuia aleji,
kulingana na jinsi daktari wako atakavyoona inafaa kutegemeana na ukali wa
tatizo, dalili zake, umri wako pamoja na hali yako ya afya kwa ujumla. Dawa
hizi ni pamoja na za jamii ya antihistamines, za jamii ya corticosteroids
ambazo ni maalum kwa kutuliza mcharuko mwili ambazo huwa katika muundo
mbalimbali kama vile cream, matone ya kuweka machoni au masikioni, za kuvuta au
kupulizia, sindano au vidonge. Kwa wale wenye mafua na kuziba kwa pua,
hushauriwa kutumia dawa zinazosaidia kuzibua pua, hata hivyo dawa hizi hazina
budi kutumiwa kwa uangalifu hasa kwa watu wenye magonjwa ya shinikizo la damu
au moyo. Dawa nyingine ni zile zinazosaidia kuzuia vitu vinavyosababisha aleji.
Nini cha kutarajia kwa mtu mwenye
aleji?
Aina nyingi za aleji hutibika kwa urahisi kwa kutumia dawa. Wapo
baadhi ya watu hususani watoto wanaweza kujenga hali ya aleji dhidi ya aina
fulani za vyakula, hali wanayoweza kuendelea nayo mpaka ukubwani. Kwa kawaida,
kitu kikimletea mtu aleji tu mwanzoni huendelea kummuathiri daima.
Kuna madhara yeyote ya kuwa na aleji?
Madhara ya aleji ni pamoja na kupata shambulio kali la mcharuko mwili ambalo
linaweza kusababisha kifo kama usipotibiwa haraka. Wapo baadhi ya watu, kwa
mfano, wakila kumbi kumbi huvimba mwili na kushindwa kupumua mpaka kuhitaji
kulazwa hospitali na kusaidiwa kupumua kwa mashine. Madhara mengine ni pamoja
na shida ya kuvuta pumzi au kushuka kwa shinikizo la damu (kupata shock).
Nitajikingaje dhidi ya aleji?
Jambo la msingi la kufahamu ni kuwa, kuwa na aleji si uchawi.
Pindi mtu anapopatwa na aina fulani ya aleji, kinga bora ni kukwepa mambo yote
yanayoweza kuchochea kutokea kwa shambulizi la aleji. Kama ni chakula, jitahidi
kukwepa aina hiyo ya chakula na kama ni dawa, acha matumizi yake na pia mueleze
daktari wako au muuguzi kuhusu hali hiyo mapema kabla hajakupatia dawa hizo
pindi unapokwenda hospitali kwa matibabu ya matatizo mengine.
Wapo watoto wachanga ambao hupatwa na aleji mara tu
wanaponyweshwa maziwa ya ng'ombe kwa mara ya kwanza. Hii hutokana na aina
fulani ya protini iliyopo kwenye maziwa haya. Ili kuwakinga wasipatwe na aina
hii ya aleji, mama hushauriwa kunyonyesha mtoto kwa angalau miezi minne ya
mwanzo huku akiepuka kumpa maziwa ya ng'ombe katika umri huu.
Baadhi ya kinamama hudhani kwamba kubadilisha aina ya chakula
wakati wa kunyonyesha kunaweza kusaidia kumuepuesha mtoto asipatwe na aleji.
Hii si kweli kwa vile imeonekana kitendo hiki hakisaidii kumkinga mtoto dhidi
ya aleji.
Uchunguzi mwingine umewahi kuonesha kuwa watoto waliozaliwa
katika mazingira ya vumbi vumbi na mifugo (yenye kiasi kikubwa cha manyonya ya
wanyama na vumbi) wana uwezekano mdogo wa kupata aleji ya vitu vya aina hii
pindi watakapokuwa wakubwa ikilinganishwa na wale waliozaliwa katika mazingira
yasiyo na hali hizo. Hii ni kwa vile, mazingira ya vumbi huwajengea watoto hawa
aina fulani ya 'kinga' dhidi ya aleji tofauti na wenzao. Hata hivyo, watoto
waliohamia katika mazingira haya wakiwa na umri mkubwa wameonekana kuathirika
kwa vile wamekosa ile kinga ya utotoni.
No comments