BIMA YA AFYA NA FAIDA ZAKE

 

Bima ya afya ni nini?

Bima ya afya ni mfumo wa kujiunga kwa hiari ama kwa lazima unaomhakikishia mwanachama kugharamiwa gharama zozote zinazojitokeza katika kupata huduma za kiafya zikiwemo kumwona daktari, kufanya vipimo pamoja na kupata matibabu na dawa kwa mwanachama husika. Bima ya afya ni kama mkataba unaoingiwa na anayetaka huduma pamoja na mtoa huduma kwa kupitia mifuko au taasisi inayowaunganisha mtoa huduma pamoja na mhitaji wa huduma husika.
Mara nyingi Bima ya afya hujumuishwa kwenye makato anayoyatoa mwajiri kwa waajiriwa wake katika kufanya malipo. Pia zipo bima zinazowahusu watu binafsi, wazee na wasiojiweza, wajawazito na wengine wenye mahitaji maalumu bila kusahau wanafunzi kipindi cha masomo yao. Mara nyingi wanachama huchagua taasisi ama mifuko inayotoa bima hizi kulingana na aina, viwango na mipaka (coverage) ya Taasisi/Bima hizo.

Ni ukweli uliowazi kuwa kila mfuko huweza kutofautiana na mingine katika huduma inazozitoa kwa mfano kwa hapa Tanzania mfuko wa NHIF (National Health Insurance Fund) ni mfuko unaotumiwa zaidi na wafanyakazi waliopo katika taasisi rasmi wengi wao wakitoka serikalini. Kwa upande mwingine kuna mifuko mingine tofauti na NHIF kama STRATEGIS, AAR, METROPOLITAN na mingineyo ambayo inafuata utaratibu ule ule wa wafanyakazi wa serikali au wa sekta binafsi kujiunga na mwajiri kuwakata kiwango fulani cha pesa kwa ajili ya wao kupata uhakika wa matibabu wao na familia zao. Kwa mantiki hiyo ni vyema kwa kila mwanchama kuwa na ufahamu wa kutosha kuhusu huduma, viwango na mipaka (limitations) ya mfuko wa bima anaoamua kuuchagua.

AINA ZA BIMA YA AFYA TANZANIA

Mfuko wa NHIF

Kwa nia njema ya kuhakikisha huduma za afya bora na nafuu kwa wafanyakazi wa serikali, mashirika binafsi na makundi mengine zinapatikana kwa wanachama wachangiaji na wategemezi wao, serikali iliangalia njia mbadala kwa kuanzisha mfuko wa huduma za afya ili kutekeleza mageuzi ya sera ya sekta ya afya (1993/3). Matokeo yake mwaka 1999 Serikali ilianzisha mfuko wa taifa wa bima ya afya kama taasisi ya umma chini ya sheria no 8 ya 1999 (Sura ya 395, kama ilivyorekebishwa mwaka 2002)
Mfumo wa uchangiaji wa mfuko hutegemea uwezo wa kulipa wa mwanachama na si vinginevyo, na kwa mujibu wa Sheria ya NHIF, wafanyakazi na waajiri katika sekta ya umma wana wajibu wa kujiandikisha na kuchangia jumla ya asilimia 6 ya mshahara wa mwezi kwa kila mfanyakazi ambayo huchangiwa kwa pamoja kati ya mwajiri na mwajiriwa. Aidha utaratibu maalumu umewekwa juu ya utaratibu wa kuchangia kwa makundi maalumu mengineyo kama vile wanafunzi, viongozi wa dini pamoja na vyama vya watu binafsi. Wanufaika wa mfuko huu ni pamoja na Mwanchama mchangiaji, mke na hadi wategemezi wanne ambao wanatambulika kisheria na kwa maana inayokubalika zaidi wategemezi ni pamoja na watoto wa damu au watoto waliorithiwa kisheria na wazazi. Hii inamaanisha kama baba au mama ameajiriwa na amejiunga na mfuko wa NHIF basi yeye na mke au mme wake pamoja na wategemezi wanne wote watapatiwa matibabu kama wategemezi wa yule aliyeajiriwa. Pia muajiri husika pamoja na wategemezi wote watapatiwa kadi za NHIF.

Mfuko wa CHF

CHF (Community Health Fund) ni mpango wa hiari ulioanzishwa kwa sheria Na. 1 ya mwaka 2001 (Sura 409 ya sheria za Tanzania Toleo la 2002) wa kaya au familia kuchangia gharama za matibabu kabla ya kuugua. Kaya katika huduma za matibabu za CHF ni pamoja na baba, mama na watoto chini ya umri wa miaka 18. Mtu yeyote mwenye umri zaidi ya miaka 18, taasisi mfano shule (wanafunzi) ushirika (wanaushirika), vikundi vya uzalishaji nk wanaweza pia kutumia mfuko wa CHF.
Ndani ya mfuko huu mwanachama atanufaika na huduma zote za msingi za kinga pamoja na tiba zitolewazo katika zahanati, kituo cha afya na hospitali ya wilaya kama vile huduma ya wagonjwa wa kutwa na kulazwa, vipimo vya maabara na pia huduma ya upasuaji kulingana na utaratibu uliowekwa na halmashauri husika. Wanachama wa CHF wanapata huduma bora ya afya mwaka mzima, ilhali halmashauri zinazoendesha mifuko hii zinapata malipo toka serikalini ambayo yanatumika kuboresha huduma za afya.

Mifuko binafsi

Pamoja na mifuko tajwa hapo juu ipo mifuko mingine ambayo kwa asilimia kubwa hutumiwa na sekta binafsi iliyo na wigo mpana zaidi wa huduma kulingana na hali ya maisha na mahitaji ya watumiaji. Mifuko hii ni kama vile STRATEGIS, AAR, METROPOLITAN na mingine. Mifuko hii inatofautiana kimikataba kutoka mfanyakazi mmoja hadi mwingine au mwajiri mmoja hadi mwingine. Baadhi ya mifuko inauwezo wa kutoa matibabu hadi yale ya gharama za juu sana ikiwemo hata kupelekwa kutibiwa nje ya nchi. Ni vyema kuuchunguza mkataba wako wa bima ya afya pale tu mwajiri wako atakapokuwa anakuandikisha ili kutambua haki yako kama mtumia huduma na mipaka ya huduma husika.

Kwa nini ni muhimu kujiunga na mfuko wa Bima ya afya?

Mkombozi wakati wa dharura
Bima ya afya ni miongoni mwa bima muhimu sana kwani kuwa nayo hukusaidia kupata matibabu hata kama hauna fedha taslimu. Hata kama umepata dharura na wasamaria wema wamekusaidia tu kukupeleka hospitali basi wakitoa kadi yako ya bima utatibiwa bure mpaka utakapopona, hakutakuwa na sababu ya kuchelewesha matibabu yako. Hivyo ni muhimu sana kuwa na bima ya afya maana itakusaidia kwa mengi hasa pindi cha dharura na pindi hali yako ya kifedha sio nzuri. Hata hivyo kama bima zilivyo ni vyema kujiandaa na kuwa tayari kwani huwezi kujua lini wewe au mtegemezi kutoka kwenye familia yako ataumwa.
Huondoa wasiwasi wa gharama za afya
Bima ya afya husaidia sana pia kukuwezesha kupata matibabu ya gharama kubwa kuliko ile ambayo ungeweza kulipia. Chukulia mfano unapata tatizo ambalo gharama yake kwa jumla ya matibabu ni Tshs 500,000/= na imetokea ghafla umepata tatizo kama ajali. Kutegemea na hali yako kimaisha, unaweza ukashindwa kupata kiwango hiki cha pesa au ikakubidi kutoa fedha zako zingine kwa ajili ya matibabu hayo. Ila ukiwa na bima ya afya hutahitajika kulipa kiwango hicho kwani ukiwa mwanachama unalipa kila mwezi tayari.

Familia yote inajumuishwa
Bima ya afya pia inakuwezesha wewe na wategemezi wako kama familia yako mkeo, watoto kupata matibabu kwa kadiri inavyowezekana na kwa michango nafuu unayochangia kwa utaratibu uliowekwa. Hii inasaidia sana kupunguza gharama na kufanikisha kuwepo kwa matumizi mazuri ya pesa kwa maana familia yako ukiwemo wewe mchangiaji mtapata huduma kila mtakapohitaji bila vipingamizi vyovyote vile.

Uhakika wa kutibiwa vituo vikubwa
Bima ya afya humhakikishia mtumiaji upatikanaji wa huduma bora za vipimo, matibabu na dawa zenye viwango bora na uhakika wa kupona. Hii ni kwa sababu mwanachama atahudumiwa hospitali zinazofahamika na zinazotoa huduma zenye viwango nchini ambazo zipo chini ya/zinazoshirikiana na mifuko ya bima ya afya. Ukosekanaji wa bima za afya hupelekea watu kwenda kupata huduma katika zahanati ndogondogo na vituo vidogo vya afya visivyo na wataalamu wa kuaminika, vifaa bora na huduma nzuri kwa ujumla na mbaya zaidi katika maeneo haya mhitaji wa huduma hulazimika kulipa fedha taslimu swala ambalo humletea hasara pamoja na kupatiwa huduma mbovu.
Ni vyema kujiunga na mfuko wa bima ya afya unaoendana na hali yako ya kimaisha ili kukuwezesha kuishi maisha yenye amani, afya bora na ya furaha.

No comments