NDIZI mbivu ni tunda linalofahamika na kila mtu, lakini sina hakika
kama watu wote wanafahamu umuhimu na faida za tunda hili ambalo
linapatikana kirahisi sana nchini.
Kama ulikuwa hujui umuhimu na
faida za ndizi mbivu mwilini, naomba usome makala haya na baada ya
kusoma naamini utakuwa na mtizamo tofauti kuhusu tunda hili.
KINGA DHIDI YA SHINIKIZO LA DAMU NA MARADHI YA MOYO
Kwa mujibu wa utafiti wa kisayansi kuhusu tunda hili, ndizi ni chanzo
kikubwa cha madini aina ya ‘Potassium’, ambayo ni muhimu sana katika
kuweka shinikizo la damu mwilini katika hali yake ya kawaida (Normal
Blood Pressure), na huboresha utendajikazi mzuri wa moyo. Ndizi moja tu
kwa siku inaweza kukukinga na maradhi ya shinikizo la damu na matatizo
ya moyo.
Ukweli kuhusu vyakula vyenye kiwango kikubwa cha madini
ya ‘Potassium’ katika kushusha shinikizo la damu mwilini, umethibitishwa
na tafiti nyingi za kisayansi. Kwa mujibu wa jarida moja la masuala ya
afya nchini Marekani, zaidi ya Wamarekani 40,000 wa kike na kiume,
walifanyiwa utafiti kwa muda wa miaka minne na ikagundulika kwamba watu
wanaokula vyakula vyenye ‘Potassium’ na ‘Fiber’ (kambalishe),
wamejiepusha na kupatwa na kiharusi.
KINGA DHIDI YA VIDONDA VYA TUMBO
Kwa muda mrefu imethibitishwa kwamba ndizi ina virutubisho vyenye uwezo
wa kupambana na asidi tumboni hivyo kutoa kinga dhidi ya vidonda vya
tumbo (Stomach ulsers) na kutoa ahueni kwa mtu ambaye tayari
ameathirika. Katika utafiti mmoja, ilibainika kwamba mtu akila
mchangayiko wa ndizi mbivu na maziwa huzuia utokaji wa asidi tumboni
inayosababisha vidonda vya tumbo.
Kwa mujibu wa utafiti wa
kisayansi juu ya suala hili, ndizi hutoa kinga na ahueni ya vidonda vya
tumbo kwa njia mbili. Mosi: virutubisho vilivyomo kwenye ndizi huzipa
uhai seli zenye kazi ya kutengeneza utandu ambao hutoa aina fulani ya
urojo (mucus) unaotumika kama kizuizi dhidi ya asidi tumboni.
Hivyo kama wewe hujapatwa na vidonda vya tumbo, kwa kula ndizi mara kwa
mara unajipa kinga madhubuti na kama tayari umeathirika na vidonda, kwa
kula ndizi utajipa ahueni kubwa.
TIBA KWA WENYE MATATIZO YA CHOO
Ndizi ni muhimu sana katika kulainisha na kusafisha tumbo na
kumuwezesha mtu kupata choo laini. Mbali ya kusaidia upatikanaji wa choo
kwa wenye matatizo hayo, lakini pia hutoa ahueni kwa wagonjwa wa
Kipindupindu. Mtu aliyepatwa na maradhi hayo hupoteza kiasi kikubwa cha
madini ya ‘Potassium’, hivyo kwa kula ndizi ataweza kurejesha mwilini
haraka madini yake yaliyopotea.
UIMARISHAJI WA NURU YA MACHO
Wakati ulipokuwa mdogo, bila shaka uliwahi kuambiwa na mama kuwa mtu
akila karoti, atakuwa akiona vizuri. Bila shaka hakukosea, lakini sasa
ukiwa mtu mzima unaambiwa kwamba ulaji wa matunda, ikiwemo ndizi ndiyo
kinga hasa dhidi ya matatizo ya kutokuona vizuri uzeeni.
Ndizi
hujenga kwenye utumbo mwembamba uwezo mzuri wa kunyonya madini ya
‘calcium’ na virutubisho vingine na hivyo kuwezesha virutubisho kuingia
mwilini na kuzunguka katika mfumo wa damu bila matatizo.
Baadhi ya vitamini na madini yaliyomo kwenye ndizi ni pamoja na Vitamini
B6, Vitamin C, ‘Potassium’, ‘Manganese’ na Fibre (kambalishe). Hivyo
utaona kwamba tunda la ndizi ni muhimu kwa sababu limesheheni vitamini
na madini muhimu katika mwili wa binadamu. Kuanzia leo itazame ndizi
kama tunda muhimu sana katika ustawi wa afya yako. Ndizi pia hutia mwili
nishati, unaposikia uchovu, kula ndizi moja na utajisikia mchangamfu.
No comments