Maji huunda karibu asilimia 70 ya mwili wa mwanadamu, hivyo umuhimu wake hauwezi kufumbiwa macho. Karibu kila kitendo kinachofanywa na mwili husaidiwa na maji kuanzia kuondoa uchafu na sumu mwilini hadi kusaga chakula. Pia maji huifanya ngozi kuwa na siha na kusafirisha virutubisho vya chakula katika mwili mzima. Kwa kawaida kuvumilia njaa katika mwezi wa Ramadhani ni jambo rahisi zaidi kuliko kuvumilia kiu. Iwapo utahisi kuwa virutubisho vya chakula na madini vimepotea mwilini kwa kutokwa na jasho sana, unapaswa kufidia mada hizo kwani kuendelea mwenendo huo kunaweza kusababisha mwili kudhoofika kufikia mwishoni mwa mwezi Mtukufu wa Ramadhani. Unaweza kufidia virutubisho, madini na maji yanayopotea mwilini kwa kula lishe inayotakiwa wakati wa kufuturu na pia daku. Zifuatazo ni njia kadhaa za kuzuia kiu wakati tunapokuwa tumefungwa.
Kwa kuzingaitia kuwa mwezi wa Ramadhani mwaka huu katika maeneo mengi duniani umeangukia msimu wa joto kali la kiangazi huku masaa ya kufunga yakiwa marefu, wanaofunga wanashauriwa ili kuzuia kuhisi sana kiu na kupunguza ukosefu wa maji mwilini, wajiepushe kutoka majumbani mwao pasipo udharura. Pia wajiepushe kupigwa na jua na kila inapowezekana wakae kwenye kivuli na maeneo yenye ubaridi. Pia kama inawabidi kutoka nje ya nyumba kwa shughuli mbalimbali basi wajitahidi kuvaa kofia za kuzuia jua huku wakijiepusha kuushughulisha sana mwili.
Pia wafungaji wanashauriwa kujitahidi katika kipindi cha saa moja baada ya kufuturu hadi nusu saa kabla ya wakati wa daku kunywa maji bilauri 6 hadi 8, huku wakiendelea kula vyakula vyenye ufumwele vinavyosaidia kuzuia kiu kwa muda mrefu. Wakati huo huo wafungaji wanatakiwa kujiepusha kunywa chai, kahawa na soda kwani vinyaji hivyo vina kiwango cha juu cha kafeini inayoufanya mwili upoteze maji kwa haraka na mfungaji kuhisi kiu zaidi.
Wanaofunga mwezi Mtukufu wa Ramadhani hasa katika maeneo yenye joto kali wanapaswa kujua kuwa, kunywa maji mengi wakati wa daku hakuzuii kuhisika kiu baadaye, kwani mwili unapohisi kuwa una kiwango kikubwa cha maji, huyatoa mwilini kupitia mkojo. Hivyo basi, maji yanayohitajika kwa ajili ya mwili yanapaswa kunywewa hatua kwa hatua kati ya wakati wa kufuturu hadi daku na pia kula matunda yenye majimaji kunasaidia suala hilo.
Vilevile baadhi ya vyakula vitamu na vyenye sukari nyingi kama kaimati na jelebi hupunguza maji mwilini na kumfanya mtu aliyefunga ahisi kiu zaidi. Pia kutozingatia suala hilo na kuongezeka ghafla homoni ya insulini katika damu hupunguza kiwango cha sukari katika damu na wakati wa mchana mfungaji anaweza kuhisi uchovu na maumivu ya kichwa. Hivyo inashauriwa kutokula vyakula kama hivyo ili kuepuka kiu. Pia kunywa maji ya matunda asilia na kula mboga na matunda yenye maji kama vile matikiti, matango na kadhalika huweza kusaidia kufidia virutubisho na maji yaliyopotea mwilini. Hivyo basi, mbali na maji pia tunashauriwa kula lishe kamili na vyakula vya makundi yote bila kusahau matunda na mboga freshi ili kudhamini mahitaji yote ya mwili na kuupatia virutubisho muhimu kama vile calcium, ufumwele, potassium na madini tofauti.
Moja ya mambo yanayowasumbua wagonjwa wengi wakati wa mfungo wa mwezi wa Ramadhani ni kujua wanywe vipi dawa zao katika mwezi huo huku wakiendelea na swaumu. Ni muhimu kwa wagonjwa wanaoweza kufunga wasipuuze kumeza dawa au kuacha tu dozi za dawa zao kiholela, kwani kufanya hivyo kunaweza kuwaletea matatizo na kuharibu mwenendo mzima wa matibabu.
Hivyo kabla ya kuchukua hatua yoyote ile kuhusiana na kubadilisha muda wa kunywa dawa wanashauriwa kupata ushauri wa daktari. Hii ni kwa sababu kukatiza ghafla dozi ya dawa kuna hatari, huku kubadilisha muda wa kumeza dawa, au kutozingatia kiasi cha dawa na muda wa kuzimeza kunaweza kuleta mabadiliko katika athari ya dawa na pia matatizo ya matibabu.
Kwa ujumla chakula kinaweza kupunguza, kuongeza au kuchelewesha ufyonzaji wa dawa mwilini. Muda wa kumeza dawa kwa kawaida hubadilika wakati wa mwezi mtukufu wa Ramadhani kwa kuzingatia muda kati ya futari na daku, na hivyo dawa huweza kumezwa kwa mujibu wa makundi mawili. Kwa wale ambao wanatakiwa kunywa dawa mara moja katika kipindi cha siku nzima yaani usiku na mchana, muda wao wa kunywa dawa haubadiliki kwa kiasi kikubwa, isipokuwa tu kama mgonjwa alitakiwa kunywa dawa mara moja mchana anaweza kubadilisha muda huo na badala yake kunywa wakati wa usiku baada ya kufuturu. Iwapo dawa zinatakiwa kunywewa huku tumbo likiwa tupu, muda muwafaka wa kumeza dawa katika hali hiyo ni saa moja kabla ya daku au masaa mawili baada ya kufuturu.
Kwa wale ambao wanapaswa kunywa dawa zao mara mbili au tatu kwa siku, pengine baada ya kupata ushauri wa daktari wanaweza kunywa dawa zao kati ya kipindi cha futari na daku. Katika hali maalumu pengine daktari anaweza kubadilisha dawa za mgonjwa na kumpatia zile ambazo zina athari za muda mrefu ili kuepusha kumeza dawa mara kadhaa kati ya vipindi vifupi. Au pia daktari anaweza kumpatia mgonjwa dawa nyingine zilizo sawa na anazotumia lakini ambazo anaweza kutumia usiku badala ya mchana ili kumuwezesha kufunga bila kukatishza dozi au kupata matatizo. Antiobiotics ni miongoni mwa dawa zinazopaswa kumezwa wakati uliopangwa na hazipaswi kubadilishwa muda wake lakini daktari pia anaweza kumpatia mgonjwa dawa mbadala ambazo ataweza kumeza bila kuathiri swaumu yake.
Wapenzi wasomaji tunapaswa kujua kuwa kubadilisha mpangilio wa kunywa dawa, aina na njia zinazofaa za matumizi ya dawa ni jambo ambalo linapaswa kuamuliwa na kuelekezwa na tabibu husika hivyo wagonjwa wanashauriwa kuhakikisha kuwa wanapata ushauri wa daktari kuhusu suala hilo.
No comments