Maumivu Wakati Wa Hedhi (Dysmenorrhea)



maumivu kabla ya hedhi

Katika mfululizo wa mada hii, tunazungumzia matatizo yanayoambatana na hedhi. Katika kurasa nyingine tutazungumzia maumivu yanayowapata wanawake kabla ya kuanza hedhi (Premenstrual syndrome), matatizo yanaambatana na kukosa hedhi (Amenorrhra) na yale yanayowapata wanawake waliokoma hedhi (Menopausal syndrome). Ukurasa huu ni mahsusi kwa matatizo ya wakati wa hedhi. Maumivu wakati wa hedhi huitwa menstrual cramps au kitaalamu Dysmenorrhea.
Menstrual cramps ni maumivu ya kukakamaa kwa misuli ya eneo la chini ya tumbo. Wanawake wengi hupata maumivu haya kabla kidogo au wakati wakiwa kwenye siku zao. Kwa baadhi ya wanawake, maumivu haya huwa ni ya kuwakosesha raha. Kwa wengine, huwa ni makubwa kiasi cha kuwafanya washindwe kuendelea na shughuli zao za kila siku kwa siku kadahaa kila mwezi.
Primary dysmenorrhea ni maumivu ya wakati wa hedhi ambayo hujirudiarudia kila mwezi na ambayo hayatokani na magonjwa mengine ya mwili. Maumivu haya ya wakati wa hedhi ambayo hayana sababu za kueleweka, hupungua kadri mwanamke anavyozidi kuwa na umri mkubwa na mara nyingi hupungua sana mara baada ya kuzaa.
Secondary dysmenorrhea ni maumivu ya wakati wa siku za mwanamke ambayo yanatokana na dosari katika viungo vya uzazi vya mwanamke, kama endometriosis, adenomysis, uterine fibroids au maambukizi ya wadudu.

Dalili Za Maumivu Ya Hedhi (Menstrual Cramps)


hedhi yenye matatizo
. Maumivu ya kukakamaa kwa misuli sehemu ya chini ya tumbo yanayoweza kuwa makali
. Kichwa kizito na maumivu ya kichwa endelevu
. Maumivu yanayenea sehemu za mgongoni na kwenye mapaja
Wanawake wengine hupata:
. Kichefuchefu
. Haja kubwa mara kwa mara
. Maumivu ya kichwa                                                                                 . . . .Kizunguzungu


Chanzo Cha Maumivu Ya Wakati Wa Hedhi


Wakati wa hedhi, nyumba ya uzazi hujiminya ili kuondoa utando wake wa juu. Vitu vilivyo mfano wa homoni – prostaglandins – vinavyohusika na maumivu na uvimbe, huchagiza kujiminya kwa misuli ya nyumba za uzazi (uterus). Uwepo wa prostaglandins kwa wingi kunahusishwa na maumivu makali ya hedhi.
Kujiminya kwa misuli ya uterus kukiwa kwa kiwango kikubwa mno, kunaweza kuziba mishipa ya damu inayoilisha nyumba ya uzazi (uterus). Maumivu yatokanayo yanaweza kulinganishwa na maumivu ya kifuani wakati mishipa ya damu ikiziba na kusababisha baadhi ya sehemu za moyo kukosa chakula na oksijeni.
Maumivu ya wakati wa hedhi yanaweza pia kusababishwa na:
. Endometriosis. Hii ni hali ambapo tishu ambazo kwa kawaida hujenga ndani ya uterus, zinajenga nje , hasa kwenye mirija ya uzazi (fallopian tubes), kwenye ovari au juu ya tishu zinazofunika pelvis.
. Uterine fibroids. Uvimbe usio wa saratani juu ya ngozi ya nyumba ya uzazi waweza kuleta maumivu.
. Adenomyosis. Hali hii ni pale tishu zinazofunika uterus zinapojijenga kwenye misuli ya kuta za uterus.
. Pelvic inflammatory disease (PID). Maambukizi kupitia ngono ya bakteria kwenye viungo vya uzazi vya mwanamke.
. Cervical stenosis. Baadhi ya wanawake wana vijitundu vidogo mno vya kwenye cervix vinavyozuia mtiririko wa damu wakati wa hedhi na kusababisha maumivu kutokana na msukumo wa ndani ya nyumba ya uzazi.

Mambo Ya Kufanya Kuondoa Maumivu Ya Wakati Wa Hedhi

Unaweza kufanya yafuatayo kujaribu kuondoa au kupunguza maumivu ya wakati wa hedhi:
. Mazoezi. Utafiti umeonyesha kuwa mazoezi ya mwili yanapunguza maumivu ya hedhi.
. Joto. Kutumbukia kwenye bafu la maji ya moto au kutumia chombo cha kupasha moto sehemu za chini ya tumbo kunaweza kupunguza maumivu ya wakati wa hedhi. Upashaji huu wa moto sehemu za tumboni unaweza kufanya kazi vizuri sawa na kutumia dawa za kuondoa maumivu haya.
. Chakula. Baadhi ya tafiti zimeonyesha kuwa matumizi ya vitamini E, omega-3 fatty acids, vitamini B-1 (thiamine), vitamini B-6) na magnesium yanaweza kuondoa maumivu ya wakati wa hedhi.



. Kuacha pombe na tumbaku. Vitu hivi vinaweza kuongeza makali ya maumivu ya wakati wa hedhi.
. Kupunguza msongo wa mawazo. Msongo wa mawazo unaweza kuongeza uwezekano wa kupata maumivu ya hedhi au kuongeza makali ya maumivu hayo.


Tiba Ya Maumivu Ya Hedhi

Maumivu ya wakati wa hedhi yana tiba. Daktari anaweza kukupa:
. Dawa za kupunguza maumivu. Daktari anaweza kukushauri kutumia dawa za kupunguza maumivu unapoanza siku zako au mara unapoanza kusikia dalili za maumivu na kuendelea kuzitumia dawa hizo kwa siku 2 au 3, hadi dalili zinapoondoka.
. Hormonal birth control. Vidonge vya kunywa vya uzazi wa mpango vina homoni inayozuia upevushwaji wa yai na kuondoa maumivu ya hedhi. Homoni hizi zinaweza kutolewa kwa njia nyingine kama sindano, kitu cha kuvaa juu ya ngozi, kitu kinachowekwa chini ya ngozi ya mkono au namna ya pete laini inayoingizwa ukeni.
. Upasuaji. Kama matatizo yako yanasababishwa na kitu kinachoeleweka kama endometriosis au fibroids, upasuaji unaweza kuondoa matatizo ya maumivu ya hedhi. Upasuaji kuondoa nyumba ya uzazi (uterus) unaweza kuwa ni chaguo endapo hufikirii kuendelea kuzaa.

No comments