ATHARI ZA MAGONJWA YA ZINAA KWA WAJAWAZITO

Magonjwa ya zinaa ni maambukizi yaenezwayo kutoka mtu mmoja hadi mwingine kwa kufanya ngono na mtu mwenye vimelea vya ugonjwa. Aina ya vimelea vinavyohusika kusababisha magonjwa haya ni kama bakteria, virusi na aina nyinginezo za vimelea vya magonjwa.
Kuna aina nyingi za magonjwa ya zinaa yanayojulikana, lakini baadhi ya hayo ni kama kisonono,  malengelenge, HIV/AIDS,Pangusa,Chlamydia, HPV(Human
Papilloma Virus),Kaswende, Trichomuniasis na mengineyo mengi.

Wanawake walio wajawazito waweza kuambukizwa magonjwa ya zinaa sawa na wanawake wasio wajawazito. Magonjwa haya ya zinaa mengi huwa hayaonyeshi dalili mtu anapoambukizwa, kwa hiyo ni vigumu wakati mwingine kwa kina mama wenye mimba kugundua kama wameambukizwa magonjwa haya.Kina mama walio wajawazito ni vyema kuhudhuria kliniki ili wafanyiwe uchunguzi wa magonjwa ya zinaa ikiwepo HIV ambayo husababisha Udhaifu wa Kinga Mwilini.Ni vyema kina mama wajawazito kufahamu madhara ya magonjwa haya kwa afya zao pamoja na mimba inayokua tumboni. Wenza wa kina mama walio athirika ni lazima nao waudhurie kliniki kwa ajili ya vipimo na matibabu.

Magojwa ya zinaa yaweza kusababisha madhara makubwa kwa mama na mtoto. Baadhi ya madhara haya yaweza kuonekana wakati mtoto anapozaliwa, lakini madhara mengine huendelea kujitokeza baada ya miezi hata miaka mingi baadaye. Ugunduzi wa mapema ni muhimu kwa kuwa maambukizi mengine ya magonjwa ya zinaa kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto yaweza kuzuiliwa endapo itagundulika mapema, mfano  yawezekana kuzuia maambukizi ya HIV kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto kwa kutumia dawa maalum ambazo mama hupewa wakati wa ujauzito.
Kaswende ni ugonjwa ambao awali kabisa huambukizwa kwa kufanya ngono,lakini waweza kuambukizwa kwa mtoto wakati wa ujauzito. Mtoto anapoambukizwa  ugonjwa huu hupelekea mtoto kupata matatizo ya kiafya. Kaswende imekuwa ikihusika na kuzaliwa kwa watoto walio njiti, mtoto kuzaliwa akiwa amekufa au hata pengine mtoto kufariki muda mfupi baada ya kuzaliwa. Mtoto akiishi na asipotibiwa huweza  kuathirika ogani za mwili kama ubongo, macho, masikio, moyo, ngozi, meno na hata mifupa. Ni vyema kila mama anayeudhuria kliniki kwa mara ya kwanza kuchunguzwa endapo ana ugonjwa huu.

Kisonono ni ugonjwa ambao huambukizwa sana katika nchi za kusini mwa jangwa la sahara.Ugonjwa huu usipotibiwa wakati wa ujauzito, waweza kupelekea mimba kutoka,mtoto kuzaliwa akiwa njiti, uzito mdogo wakati wa kuzaliwa, chupa ya uzazi kupasuka kabla ya wakati na uambukizi wa majimaji yaliyomzunguka mtoto. Mtoto anaweza kuambukizwa ugonjwa huu wakati wa kuzaliwa wakati anapotoka kupitia njia ya uzazi. Mtoto asipotibiwa anaweza kupata uambukizi wa macho.

Trichomoniasis ni uambukizi katika uke wa mwanamama unasababishwa na kimelea kijulikanacho kama Trichomona vaginalis.Dalili za ugonjwa hutofautina kutoka mwanamama mmoja hadi mwingine. Lakini dalili zinapojitokeza huwa ni kuwashwa sana,harufu mbaya, kutoka majimaji yenye harufu na kutoka damu baada ya tendo la ndoa. Kina mama wenye dalili za ugonjwa ni vyema kuchunguzwa na kupatiwa matibu sahihi. Uambukizi usiotibiwa unahusishwa na kujifungua kabla ya wakati,kupasuka chupa ya uzazi kabla ya wakati na mtoto kuzaliwa akiwa na uzito mdogo.Ni mara chache mtoto huambukiazwa ugonjwa wakati wa kuzaliwa.

Ugonjwa mwingine ni Hepatitis B ambao ni uambukizi katika ini usababishwao na virusi aina ya Hepatitis B (HBV).Mama anaweza kumuambukiza mtoto wakati wa ujauzito, na hatari ya uambukizi hutegemea ni wakati gani mama aliambukizwa ugonjwa. Hatari huwa kubwa endapo mwanamama ataambukizwa ugonjwa anapokaribia kujifungua.Mtoto mwenye ugonjwa kwa muda mrefu huwa katika hatari ya kupata ugonjwa sugu wa ini au hata saratani ya ini baadaye katika maisha yake.Uambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto waweza kuzuiwa kwa upimaji wa mapema pamoja na kutoa tiba kwa mtoto mara baada ya kuzaliwa.

Hepatitis C ni uambukizi wa ini usababishwao na virusi vya Hepatitis C (HCV), na huweza kuambukizwa kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto wakati wa ujauzito.Mara nyingi ugonjwa hupimwa kwa wale walio katika hatari ya kuambukizwa ugonjwa huu, mfano wale wanaojidunga dawa za kulevya. Athari za ugonjwa huu ni mama kujifungua kabla ya wakati na mtoto kuzaliwa akiwa na uzito mdogo.Kwa kawaida watoto wanaoambukizwa huwa hawaonyeshi dalili, na ugonjwa waweza kuisha wenyewe bila kutibiwa na hata kama ugonjwa utajitokeza, huwa ni rahisi kuutibu kwa watoto ukilinganisha na watu wazima.
Upimaji, pamoja na matibabu ya magonjwa ya zinaa ni muhimu kwa afya ya mama mjamzito na mtoto atakayezaliwa. Kwa hiyo ni jukumu la wazazi kujilinda na kujikinga na magonjwa haya kwa ajili ya afya yao na watoto watakaozaliwa.

Ni vyema kwa kina mama wajawazito kuzungumza na daktari wao kuhusu kufanyiwa vipimo vya magonjwa haya. Pia kujadili dalili wazipatazo ambazo zinahusiana na magonjwa haya ya zinaa au endapo walijihusisha na vitendo vya ngono isiyo salama. Hii ni muhimu kwa huwa ni nadra kwa magonjwa haya kufanyiwa uchunguzi, bali uchunguzi hufanyika wakati mgonjwa anapoonyesha dalili na kusubiri dalili ugonjwa hugundulika wakati umekuwa sugu.
Magonjwa ya zinaa hutibika, wajawazito walioambukizwa magonjwa kama chlamydia, kisonono,kaswende na trichomoniasis hutibiwa kwa kutumia dawa za kuandikiwa na daktari za antibiotiki ambazo  ni salama kwa wajawazito. Magonjwa yasababishwayo  na virusi hutibiwa kwa dawa za virusi (antviral medications), na juhudi mahususi uchukuliwa kuzuia maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto, kwa kutumia dawa maalum apewazo mama wakati wa ujauzito.

No comments