Mambo muhimu kuhusu unyenyeshaji wa mtoto.

KATIKA zama hizi tunazoishi,
kumekuwepo na tabia ya baadhi ya
akina dada kukataa kunyonyesha
watoto wao kwa sababu hizi na zile.


Wengine hunyonyesha kwa siku chache
sana kisha wanawaachisha watoto. Japo
imekuwa ikisisitizwa sana umuhimu wa
maziwa ya mama kwa mtoto lakini
wengi wamekuwa hawaelewi vyema
umuhimu huo ni upi. Hata mbinu za
kunyonyesha pia wengine hawazijui
vyema.

Makala haya yanajaribu,
japo kwa kifupi, kujibu au kufafanua
hoja hizo pamoja na nyingine nyingi.
Kunyonyesha mtoto maziwa ya mama, ni
tendo la asili kwa akina mama na
watoto. Kwa taratibu zetu Tanzania na
hata nchi jirani ya Kenya, mama
anapaswa kunyonyesha mwanawe
maziwa kwa miezi sita bila kumpa
chochote.

Pamoja na uasili huo, si kila mtu anajua
vyema kufanya tendo hili kwa usahihi
wake pale anapojifungua mtoto hata
kama ni mtoto wa pili! Umuhimu wa
kujua mambo kama haya, kwa mujibu
wa wataalamu, si kwa mama tu, bali
hata kwa baba na ndio maana siku si
wanawake tu wanaojifungua ndio
wanaopewa likizo ya uzazi (kama
wameajiriwa) bali hata wanaume, japo
siku ni siku tatu, lakini lengo si kwenda
kulala bali asaidiane na mkewe kulea
mtoto na kukesha! Ni muhimu kwa mtu
kujua japo kidogo namna matiti ya
binadamu yanavyoweza kuzalisha
maziwa.

Pia ni vyema kujua namna mtoto
anavyovuta ama kutumia maziwa hayo
na baadhi ya mbinu bora za
kunyonyesha mtoto kama
tutakavyoziangalia baadaye.

 KWA NINI
MAZIWA YA MAMA NI BORA?
Wataalamu wanatoa faida nyingi kwa
mtoto kunyonya maziwa ya mama yake
na hata kwa mama mwenyewe. Baadhi
ya faida ambazo zimehakikishwa
kuhusu maziwa ya mama ni kama
zifuatazo: Mosi, maziwa ya mama ndio
yana virutubisho vinavyotakiwa kwa
mtoto kuliko mengine.

Wataalamu wanasema kwamba maziwa
ya mama ndio yanayotoa nguvu halisi
zinazotakiwa kwa mtoto, protini,
vitamini, madini, na mafuta kwa vile
mtoto huyo aliyezaliwa anahitaji sana
vitu hivi ili kumwezesha kila kiungo
katika mwili wake kukua vyema.

Pili,
maziwa ya mama huwa na kinga za
mwili ambazo humsaidia mtoto
kupambana na maambukizo.
Kinga za mwili ambazo mtoto huzipata
kupitia maziwa ya mama yake
humuongezea mtoto kinga za mwili
wake dhidi ya magonjwa ya masikio,
mfumo wa uvutaji hewa kama vile
vichomo (nimonia), pamoja na
uambukizo wa magonjwa katika mfumo
wa chakula ambayo husababisha
kumpunguzia magonjwa kama
kuharisha na kuhara ama kushindwa
kupata haja.

Maziwa ya mama pia hupunguza
uwezekano wa mtoto kupata mzio,
meno kuoza, magonjwa ya moyo na
unene wa baadaye katika maisha yake
ingawa namna ambavyo ulinzi wa
maziwa unavyomsaidia mtoto ukubwani
haujulikani vyema.

Tatu, maziwa ya mama ni rahisi
kuyeyuka kuliko maziwa mengine ya
kwenye makopo na hata ya ng'ombe.
Virutubisho vilivyomo kwenye maziwa
ya mama ni rahisi kunyonywa na
matumbo ya mtoto ili kufanya kazi
mwilini kulinganisha na yale ya kwenye
makopo.
Vile vile, vimeng'enya vilivyomo kwenye
maziwa ya mama husaidia matumbo
yake kusaga chakula na kukiyeyusha
haraka mwilini.

Na hata inasemekana kuwa watoto
wanaonyonyeshwa na mama huwa na
harufu ya kupendeza isiyokifu kama
wale wanaotumia maziwa ya makopo.
Faida za kunyonyesha kwa mama Mosi,
kunyonyesha maziwa kunamsaidia
mama kupunguza uzito. Kinachofanyika
ni kwamba kunyonyesha huunguza
mafuta ambayo mwili wa mama
ulilazimika kuyahifadhi wakati wa
ujauzito.

Hivyo, mama anaponyonyesha mafuta
yanayounguzwa humrejesha haraka
katika hali aliokuwa nayo kabla ya
kushika mimba.
Hata hivyo, isichukuliwe kwamba
kunyonyesha ni moja ya mbinu
mahususi za kupunguza uzito na hivyo
kujinyima chakula! Kwa kawaida, mama
anayenyonyesha anahitaji kuongezea
kalori za chakula zinazofikia 300 au 500
ya zile anazokula mtu wa kawaida kwa
sababu anahitaji nguvu zaidi.
Pili,
kunyonyesha kunapunguza uwezekano
wa kuugua baadhi ya aina za saratani.
Idadi ya wanawake wanaogua saratani
ya uzazi au ya ziwa ni ndogo kwa
wanawake wanaonyonyesha sawasawa
kulinganisha na wale wasionyonyesha.

Tatu,
kunyonyesha mtoto kunaimarisha
mifupa ya mama. Utafiti unaonesha
kwamba mifupa inakuwa imara zaidi
pale mama anaponyonyesha mtoto na

nne,
kunyonyesha huongeza ukaribu
zaidi wa mtoto na mama yake.
Faida tele Kimsingi, mama
anaponyonyesha mwanawe maziwa,

faida zifuatazo zinapatikana:
Moja,
gharama yake ni kidogo na ni tendo
rahisi kulifanya kulinganisha na
unyonyeshaji wa kutumia chupa. Kama
mama unamnyonyesha mwanao
maziwa yako, hakuna haja ya kununua
maziwa mengine wala kusumbuka na
mipira pamoja na chuchu zake.
Pia masuala kama ya kununua mkaa,
kuni ama kumaliza uniti za umeme kwa
kuchemsha maji unakuwa huna haja
nayo.
Pili,
mama anaweza
kumnyonyesha mwanawe muda
wowote na mahala popote.
Maziwa ya mama ndiyo yanayopatikana
mahala popote mama anapokwenda na
mwanawe, na hivyo anaweza
kumnywesha kila unapoona ana dalili za
kusikia njaa.

Tatu,
maziwa ya mama
yameonesha kwamba husaidia hata kwa
watoto walizi.
Pale anapolia lia bila mpango, kazi ya
mama ni kumwekea nyonyo mdomoni
na wengi hutulia na kuchangamka.

KWA
NINI MIEZI SITA?
Wataalamu wa afya ya
mama na mtoto wanasema kwa vile
maziwa ya mama ndiyo yenye vipimo na
virutubisho sahihi anavyohitaji mtoto
kwa ajili ya makuzi yake, wanashauri
mtoto kunyonya maziwa ya mama pekee
kwa muda wa miezi sita. Wanasema
kuanzia muda huo, taratibu mtoto
anaweza kuanzishiwa vyakula vilaini
kidogo vyenye madini ya chuma baada
ya miezi sita hadi mwaka mmoja.
Wataalamu wanasema kwa uchache
sana mtoto anapaswa kunyonya maziwa
ya mama angalau kwa miezi 12. Lakini
anaweza kuendelea kunyonya hadi
miezi 36.

Ingawa hakuna utafiti unaoeleweka
kufanywa Tanzania, lakini nchini
Marekani imegundulika kwamba
wanawake wengi angalau hunyonyesha
watoto kwa miezi sita na kuwaachisha
ziwa, jambo ambalo wataalamu
wanasema si zuri kwani linaathiri afya
na makuzi mema ya watoto, labda kama
mama ana matatizo na maziwa yake.
Inashauriwa kwamba kwa vile hakuna
'fomula' yoyote ya maziwa ambayo
inaweza kulingana na yale ya mama kwa
virutubisho,

INASISITIZWA
sana akina
mama kuwanyonyesha watoto wao
maziwa yao hata kama wanafanya kazi
ama wamewaweka kwenye vituo
maalumu. Inasisitizwa pia kujifunza
kukamua maziwa na kutunza kabla ya
kwenda kazini (breast pumping).
Mbinu za kunyonyesha Inachukua muda,
hasa kwa mama 'mpya' kujua mbinu
bora za kumnyonyesha mwanawe na
kumfanya mtoto kufurahia huku na
mama mwenyewe akifurahia na bila
'kuumiza' afya yake.

Kwa wasichana ambao uzazi kwao ni
wa kwanza wanashauriwa kuwa na
mwalimu ambaye ana uzoefu, hususan
mama watu wazima. Hata hivyo, hapa
chini zipo mbinu kadhaa za kufanya
kama kianzio cha kuwasaidia:

Mlishe mapema.
Wakati unaanza, mpe
maziwa mwanao mara tu anapolia.
Kaa
mustarehe.
Ili usipate maumivu chini ya
mgongo, usijikunje sana kupeleka ziwa
kwa mwanao. Badala yake mnyanyue
mwanao karibu na maziwa.
Pendelea kukaa kwenye kiti ambacho
unaweza kuegemeza mgongo wako
raha mustarehe.
Mbinu nyingine ni
kulala ubavu huku mwanao pia akiwa
amelala upande wa pili akikuangalia.
Unaweza pia ukawa unatumia mbinu
hii, si usiku tu wakati wa kulala, bali hata
mchana kama uko nyumbani.
Hakikisha kidevu cha mwanao kimegusa
ziwa kwani inaaminika ndipo anaweza
kuvuta maziwa vizuri.

Vaa nguo
zisizobana mwili.
Inashauriwa kwa
mama anayenyonyesha kuvaa nguo
zisizobana, na zenye vishikizo mbele
ambapo ni rahisi kwake kufungua
vishikizo na kumnyonyesha mwanawe.
Pamoja na hayo kuna baadhi ya nguo
kama T-Shirts zisizobana mwili ambapo
pia unaweza kuzinyanyua juu kabisa ya
maziwa na kumnyonyesha mwanao.
Mwache mwanao apumzike.

Elewa
kwamba, kumnyonyesha mwanao ni
tendo ambalo linampa virutubisho vya
mwili na kumstarehesha pia. Mwanao
anaweza kusimama kunyonya wakati
wa kumnyonyesha ili kupumzika.
Wakati huo anaweza akawa
anakuangalia ama anaangalia chumba.
Hili si tatizo kwamba ana matatizo ya
kunyonya bali ni kupumzika tu, na mara
utamuona anaanza tena kuvuta maziwa.
Epuka kumnyonyesha mwanao haraka
haraka kwa vile una haraka.
Kunyonyesha lazima kupangiwe muda
na lazima mama pia uwe unafurahia
tendo hilo kwamba linamfurahisha
mwanawe na kuwaweka karibu zaidi.
Kwa hiyo ukishaketi kunyonyesha
achana na mambo mengine na
ikiwezekana mawazo yako yote yawe
hapo hadi mwanao atakapomaliza
kunyonya.

Mpe nyonyo zote mbili Mpe mwanao
anyonye manyonyo yote mawili wakati
unanyonyesha. Unachotakiwa kufanya
kwanza ni kuhakikisha kwamba
unampa nyonyo moja mpaka pale
utakaposikia limekuwa laini, kisha umpe
la pili.
Lakini kabla ya kumpa la pili, mpumzishe
kidogo na kumfanya acheue (wengi
wanajua namna ya kumfanya mtoto
acheue). Mjue mtoto wako ana tabia
gani anaposhiba na kufuata utaratibu
huo. Watoto wengi wanaposhiba,
huacha kuvuta maziwa, husinzia ama
kujitoa kwa mama yao.

Kausha na kusafisha chuchu. Chuchu
zako zinaweza kuwa zinauma katika
wiki chache za mwanzo. Tena zinaweza
kuwa zinauma kiasi cha kukufanya
usiwe na raha.
Lakini hili ni jambo la kawaida ambalo
huisha baada ya muda fulani. Kadhalika
unatakiwa kuhakikisha kuwa chuchu
zako zinakuwa safi muda wote, kwani
zinaweza kuwa chanzo cha magonjwa,
hususan ya kuhara kama ukiwa mchafu.
Usinywe/kula vyakula vyenye caffein
sana.

Vyakula vyenye caffein (kama vile
kahawa ama baadhi ya soda kama Coke)
vinaweza kuleta taabu kwa mtoto
(kupitia maziwa yako).
Hivyo unaweza kupunguza kunywa vitu
vya aina hiyo, ama kunywa kwa kiasi
kidogo sana. Ikiwezekana acha kabisa.
Usivute sigara ama kunywa pombe.
Kwa ajili ya afya yako na ya mtoto,
inashauriwa, tena sana, kuacha kuvuta
sigara ama hata kuwa karibu na moshi
wa mvuta sigara ama moshi wa vitu
vingine kama ule wa kiwandani.
Sambamba na hili, epuke kuwa maeneo
yenye harufu kali za kemikali. Vilevile
acha kunywa pombe kwa sababu
tindikali iliyomo inaweza kwenda hadi
kwa mtoto kupitia maziwa na kumletea
madhara, sasa au baadaye.

Jihadhari kunywa dawa kwa wingi.
Kabla ya kutumia dawa yoyote lazima
uisome maelezo na maelekezo yake
kuona kama ina madhara kwa
anayenyonyesha au la. Na hasa
unatakiwa kuongea na daktari wako
kabla ya kutumia dawa yoyote katika
kipindi cha kunyonyesha.

Angalia kile
unachokula. Kama unahisi kwamba
mwanao hupata tatizo fulani kutokana
na chakula unachokula - kama vile
anapata ukurutu kwenye ngozi ama
kuharisha kila unapokula chakula fulani-
basi kiache chakula hicho kwa muda ili
kuona hali ya mwanao. Lakini tafiti
mbalimbali zinaonyesha kuwa vyakula
freshi, hususan mboga na matunda ni
muhimu sana kwa mama
anayenyonyesha.
Ongea na daktari
wako kama kuna umuhimu wa kutumia
vidonge vya ziada vya vitamin wakati wa
kunyonyesha.
Usitegemee kuanzisha ratiba
inayoeleweka kuhusu nyakati za
kumnyonyesha mwanao hasa katika
wiki za kwanza kwanza. Si jambo rahisi
mtoto katika siku za kwanza
kunyonyeshwa hadi mara 12 kwa siku.
Hii inatokana na ukweli kwamba
matumbo yao huwa bado madogo.
Lakini kadri wewe na mwanao
mtakavyozidi kuwa pamoja huku tumbo
lake likipanuka, baadaye mtajikuta
mkiwa na ratiba kamili ya kunyonyesha.

Tafuta msaada/ushauri Kama kwako
ndio mtoto wa kwanza, au mwanzoni
ulipata matatizo katika kunyonyesha,
ama ulikuwa ukijiendea endea tu, basi
tafuta ushauri kwanza kwa wajuzi.
Kunyonyesha kunahitaji ujuzi/uzoefu na
pengine majaribio. Watu ambao
unaweza kuongea nao, ni wanawake
waliozaa zamani, hususan watu wazima
(wanawake wasomi ni bora zaidi);
wauguzi wa hospitalini ama mtaani
kwako (kama wapo), daktari wa watoto
na kadhalika.

No comments