Swali:
Mwanang Ana Umr Wa Mwaka Mmoj Na Miez Mitatu Ila Tatzo Lake Hapend Kula Kabisa Yeye Mda Wote Anahtaj Kunyonya tu
Jibu: Pole ndugu msomaji kwa tatizo linalomsumbua mwanao. Hili ni tatizo linawapata watoto wengi, hasa wanapokuwa wameanza kula vyakula vya kulikiza (weaning).
Zipo sabababu mbalimbali zinazojitokeza mara kwa mara na kumfanya mtoto kutopenda kula au kuwa msumbufu wa kula vyakula vya kawaida. Sababu hizo ni kama ifuatavyo:
Matatizo ya kiafya
Tatizo la kiafya linaweza kuwa sababu ya mtoto kukataa kula chakula. Matatizo kama haya katika jamii yetu ni magonjwa kama vile malaria. Ugonjwa huu ni moja ya sababu kwa sababu huathiri mfumo wa chakula, hivyo kukosa hamu ya kula kwa mtoto.
Matatizo mengine ni kama vile tumbo kujaa gesi na hali ya tindikali tumboni kuwa juu, kukosa choo kwa muda mrefu.
Mambo mengine ni mafua makali, vidonda mdomoni, fangasi za mdomoni, na vidonda vya koo.
Pia, uwapo wa magonjwa sugu, kuumwa mara kwa mara, hasa watoto wenye upungufu wa kinga mwilini.
Kutokua na shauku au hisia
Mtoto anaweza kuwa na hisia tofauti mwilini mwake, watoto huwa na tabia ya kutafuna vitu ambavyo siyo vyakula kwa ajili ya kujikuna fizi ili kupata nafuu mdomoni.
Mara nyingine huwa ni kama tabia iliyojijenga kama mazoea kwake na kuwa ni kiburudisho chake, pia kufanya hivi, inaweza kuwa ni mbinu ya kujihami na kutotaka kula.
Mtoto anaweza kuwa na hisia kuwa chakula kina madhara, labda akila kitamdhuru. Anaweza kuhisi kuwa akila anatapika au atagokwa na pengine akawa na woga wa kutopenda mdomo wake uguswe na chakula. Pia kutopenda ladha, harufu au mwonekano wa aina fulani ya vyakula.
Utafunaji na umezaji
Inaweza ikatokea mtoto akawa na mazoea ya kunyonya na kunywa maziwa mengine, huku bado hajajifunza vyema namna bora ya kutafuna na kumeza vyakula.
Hili ni tatizo hasa pale linapokuja suala la kula chakula, inamuwia vigumu kukitafuna na kumeza, hivyo hukijaza mdomoni katika mashavu.
Unaweza ukagundua hili kwa mwonekano wa mdomo wa mtoto, kupaliwa au kugokwa. Hali hii husababishwa na chakula kutotafunwa vizuri mdomoni.Mambo kama haya humfanya mtoto kutopenda kula.
Mpangilio wa muda wa kula
Kama mtoto umemzoesha kupata mlo muda fulani, hujijengea mazoea ya kula muda huo. Wazazi wengine wameijenga tabia hii katika familia kuwa muda fulani wazazi au walezi na watoto hula pamoja.
Unapofika muda huo mtoto huwa na dalili zakuhitaji kula. Kumchelewesha kupitiliza au kumuwahisha huweza kumuathiri ulaji wake, kwani tayari anakuwa amezoea kupata mlo muda fulani.
Tabia
Mtoto hata kama hajui kusema au kujieleza, huweza kulia au kupiga kelele zisizoeleweka ili kudai au kukataa kitu fulani. Wapo baadhi ya watu hudhani ni tabia ya mtoto kutopenda kula na kuchukulia ni utundu.
Watu huwa na imani kuwa mtoto anajifanyisha, wakati uwezekano ni dalili ya kutopenda kula zilizosababishwa na mzazi au walezi kwa kutokuwa makini katika kumlea.
Mfano, watoto wenye historia ya kula vitu visivyokuwa chakula, kama vile nguo, mpira au plastic, wengi wao huwa na tatizo la kutopenda kula.
Kama mzazi au mlezi hakumwelekeza au kumfundisha kuacha ulaji wa vitu kama hivyo mapema, tabia hii hujengeka kwa mtoto kwa muda mrefu.
Wazazi na walezi mara nyingi hujiamulia kwenda katika maduka ya dawa na kununua dawa za vitamini B pasipo kupata ushauri wa wataala wa afya wakiamini ndio suluhisho la tatizo hili.
Inawezekana kabisa ukawa umetumia muda mwingi na fedha nyingi kwa ajili ya maandalizi ya chakula cha mtoto. Pale anapogoma kula wazazi wengi hukasirika na hata kuanza kumpiga ni mkosaji.
Wengine huamua kumtisha kwa fimbo na wakati mwingine hudiriki hata kumchapa ili kumlazimisha kula. Hii siyo sahihi kabisa. Kumwadhibu kunamfanya aone kuwa wakati wa kula ni shinikizo kwa wanafamilia, hivyo hujijengea kiburi.
Yapo mambo ukiyafanya yanaweza kukupunguzia kadhia hiyo na kumfanya mtoto kupenda kula bila kushinikizwa.
Kuwa mtulivu na mpongeze
Mzazi unapaswa kuwa mpole na mtulivu huku ukificha hasira zake pale mtoto anapogoma kula au kumeza chakula. Kumbuka kitendo cha mtoto kupata njaa ni lazima atahitaji kula.
Endapo akigoma kula fahamu kuwa ameshiba au amechoshwa na aina ya chakula unachompa. Jaribu kumwacha kidogo huku ukionyesha upendo, mpe tabasamu na mfanye awe rafiki na onyesha kuwa unamjali. Akiwa katika hali ya kukufurahia jaribu tena kumlisha, akikataa fanya hivyo baada ya saa kadhaa kupita.
Badilisha vyakula
Kuwa mbunifu kwa kubadili aina za vyakula. Inawezekana mtoto amechoshwa na aina moja ya chakula, jaribu aina nyingine za vyakula na huweza kumpa ladha tofauti itakayomvutia na kumfanya akipende chakula hicho.
Wakati mwingine umbile la baadhi ya vyakula huweza kuwa kero kwa mtoto wakati wa kula. Watoto wengi hupendelea kula mlo tepetepe, laini na rahisi kutafuna na kumeza. Ni vema kuhakikisha chakula kama viazi, ndizi na ugali vimekuwa tepetepe na laini wakati wa kiviandaa.
Boresha mazingira ya ulishaji
Mazingira ya ulishaji yanaweza kuwa chanzo cha mtoto kusumbua kula chakula, mfano kama mtoto atakuwa na ndugu zake waliomtangulia, huwa na kawaida ya kucheza naye hivyo wakati wa kula wanaweza wakawa wanamvuruga katika michezo anayoipenda.
Ni vizuri mazingira yakawa tulivu na kumweka mbali na ndugu zake waliomtangulia wakati analishwa kwa sababu anakuwa na shauku ya kucheza nao. Njia nyingine ni ya kula pamoja na wenzake.
Epuka vitafunwa kabla ya muda
Ipo tabia ya baadhi ya wazazi huwa na kawaida ya kumpa mtoto vyakula vidogovidogo kama pipi, chocolate, biskuti, juisi, soda, kashata na ubuyu.
Vitu kama hivi humvurugia hamu ya kula. Ni vema kuviepuka vyakula hivyo kabla ya mlo. Unaweza ukawa unampa matunda au juisi za asili kabla ya mlo.
Mjenge kitabia
Akili ya mtoto ni kama karatasi nyeupe inayosubiri kuandikwa. Tabia ya mtoto hujengeka ndani ya mazingira anayoishi, mtindo wa kiasili wa kumwacha mtoto kuwa huru kula na ndugu au wazazi humjengea mtoto hulka ya kula.
Kufanya hivyo kunamfanya mtoto kuwa mlaji wa vyakula vya aina mbalimbali na kuvizoea. Kitendo cha kumtengenezea chakula maalumu, humfanya adhanie labda mlo wake ni tofauti na wa familia na hapo hujihisi kutengwa na kutofautiana naye.
Haya yakishindikana fika katika huduma za afya na mtoto kwa ajili ya uchunguzi na ushauri.


No comments