Tete kuwanga ni ugonjwa ambao unaombukiza nakusababishwa
na virusi vinavyojulikana kama Varicella zoster virus.Maambukizi ya tete
kuwanga huonekana sana kwa watoto wadogo ingawa hata watu wakubwa pia hupata
maambukizi ya ugonjwa huu. Tete kuwanga hupatikana duniani kote.Katika nchi
zenye kupata majira ya baridi, maambukizi ya ugonjwa huu huonekana sana wakati
wa kipindi cha majira ya baridi na kipindi cha masika.
Watoto walio na umri wa miaka 4-6 wako kwenye hatari kubwa
ya kupata maambukizi ya tete kuwanga na ndio katika umri huu ambapo maambukizi
ya ugonjwa huu yapo kwenye kiwango cha juu sana.Inakadiriwa ya kwamba, tete
kuwanga huambukiza kwa kiwango cha asilimia 90.
Watoto wengi hupata maambukizi ya tete kuwanga kabla ya
kufikia umri wa kubaleghe ingawa asilimia 10 ya vijana bado wanakuwa kwenye
hatari ya kupata maambukizi ya tete kuwanga. Katika nchi za tropiki,maambukizi
ya tete kuwanga huonekana kwa watu wakubwa na huenda yakawa maambukizi ya
hatari sana.
Maambukizi ya tete kuwanga hupatikana vipi?
Tete kuwanga huambukizwa kupitia njia ya hewa au endapo mtu
atagusana mwili na mgonjwa wa tete kuwanga(kupitia majimaji yanayotoka kwenye
vipele vya mgonjwa).Mtu yoyote yule anaweza kuambukizwa ugonjwa huu kutoka kwa
mgonjwa wa tete kuwanga kwa njia ya kucheka, kupiga chafya, kukohoa .Hii
inatokana na kusambazwa kwa virusi ya Varicella zoster kwa njia ya hewa pindi
mgonjwa anapocheka,kupiga chafya au anapokohoa.
Nini hutokea kipindi cha maambukizi (Pathofiziolojia)
Maambukizi ya tete kuwanga kwa mtoto husababisha mtoto
kutoa kinga aina ya Immunoglobulin G (IgG), Immunoglobulin M, (IgM) na
Immunoglobulin A,(IgA). Kinga hizi pamoja na kinga zinazosaidiwa na chembechembe
za mwili (Cell mediated responses)husaidia kupunguza
madhara na urefu wa maambukizi haya ya awali ya tete
kuwanga.Immunoglobulin G hubakia kipindi chote cha maisha na huweka kumbukumbu
ya maambukizi ya tete kuwanga na hivyo kuwa chanjo dhidhi ya ugonjwa huu hapo
baadae maishani.Baada ya kupata maambukizi ya Varicella zoster virus, virusi
hivi husambaa hadi kwenye tishu za ngozi, kamasi (mucosal) na hata kwenye
mishipa ya fahamu (sensory nerves).Virusi hivi baada ya
muda huwa kimya (dormant) {‘’ambapo ndio tunasema mgonjwa
amepona’’} kwenye kifundo cha mishipa ya fahamu vinavyojulikana kama dorsal
ganglion of sensory nerves.Kuchepuka tena kwa virusi hivi ambavyo awali
vilikuwa vimekaa kimya ndio husababisha ugonjwa wa ukanda wa jeshi (herpes
zoster),postherpetic neuralgia, na Ramsay Hunt Syndrome Type II.
Ramsay Hunt Syndrome type II inaambatana na dalili za
kupooza sehemu mbalimbali za uso,maumivu kwenye sikio/masikio, kupoteza ladha
ya ulimi (taste loss),mdomo kukauka, macho kuwa makavu na vipele kwenye mwili.
Dalili na viashiria vya Tete kuwanga
Dalili za kwanza ni;
• Kichefuchefu
• Kupungua kwa hamu ya kula
• Maumivu ya kichwa
• Maumivu ya misuli
• Kuumwa tumbo
Dalili hizi baadae hufuatiwa na hatua ya mgonjwa kutoka
vipele, uchovu na homa ambayo sio kali sana, hatua hii ndio huonyesha kuwepo
kwa ugonjwa wa tete kuwanga.
Vipele hivi mwanzo huonekana kama alama nyekundu ndogo
kwenye uso, kichwa, tumbo,kifua, sehemu za juu za kwenye mikono na miguu ambapo
baada ya masaa 10-12 alama zile nyekundu hugeuka kuwa uvimbe, uvimbe huu kisha
hujaa maji na kupasuka. Baadae vipele vipya (blisters) huanza kuchipuka kwa
makundi kwenye sehemu za tupu ya mwanamke (vagina), kope (eyelids) na mdomoni
ambavyo hupasuka na kuwa vidonda vidogo vidogo kwenye sehemu hizi.
Hatua hii ya kutokea vipele huanza kuonekana kuanzia siku
ya 10-21 baada ya mtu kupata maambukizi ya Varicella zoster virus na huambatana
na kuwashwa sana mwili.Vipele vinaweza kutokea kwenye viganja vya mkono, nyayo
na hata kwenye pua, lips, masikio, njia ya haja kubwa.
Vipele venye majimaji (blisters) hutokea siku ya 4-7 baada
ya hatua ya kutoka vipele kuanza na hupotea kuanzia siku ya 5 na kuendelea.
Mtu ambaye ana maambukizi ya tete kuwanga huweza kuambukiza
watu wengine siku moja au mbili kabla ya kuanza kutoka vipele na kuendelea kuwa
na uwezo wa kuambukiza wengine kwa siku 4-5 baada ya vipele kutokea.
Dalili ya kwanza ya tete kuwanga kwa watoto ni vipele kabla
ya dalili nyingine nilizotaja awali hapo juu kufuata.Kwa watu wakubwa, vipele
husambaa katika maeneo mengi mwilini kwa wingi na homa huwa ya muda mrefu sana
na pia huweza kupata homa ya mapafu inayosababishwa na virusi vya Varicella
zoster virus.
Baadhi ya watoto ambao walipata chanjo ya ugonjwa huu hapo
awali huweza kupata tena maambukizi ya tete kuwanga ingawa yanakuwa sio makali
sana(hutoka vipele 30 kwa wastani) lakini watoto hawa bado wana uwezo wa
kuambukiza wengine ugonjwa huu.Kwa kawaida mtoto hutokea wastani wa vipele 250
hadi 500 wakati wa maambukizi ya ugonjwa wa tete kuwanga.
Ugonjwa huu ni nadra sana kuwa na madhara makubwa ingawa
madhara huweza kuonekana kwa wagonjwa walio na upungufu wa kinga mwilini, wenye
kuugua magonjwa sugu au wanawake wajawazito ambao hawakupata chanjo ya ugonjwa
huu.
Vipimo vya uchunguzi
I. Utambuzi wa ugonjwa huu hufanywa kwa kuangalia dalili na
viashiria vya ugonjwa huu(Kichefuchefu, kupungua kwa hamu ya kula,maumivu ya
kichwa,maumivu ya misuli, kuumwa tumbo na vipele)
II. Kupima majimaji ya ndani ya vipele kwa kutumia direct
immunoflorescent test
III. Kipimo cha damu kuangalia wingi wa Immunglobin M
(IgM), ambapo kiwango chake huongezeka panapotokea maambukizi mapya au
kuangalia uwepo wa Immunoglobulin G (IgG) ili kuthibitisha kuwepo kwa
maambukizi hapo awali.
IV. Kipimo cha ultrasound kwa wanawake wajawazito ili
kuangalia dalili za kuwepo kwa maambukizi ya ugonjwa huu kwa kiumbe kilichomo
tumboni (Fetal Varicella Infection).Inashauriwa kuchelewesha kipimo hiki kwa
wiki 5 toka mama apate maambukizi ya tete kuwanga ili kuweza kutambua kama
mtoto ameathirika au la.
V. Kipimo cha kuangalia vina saba (DNA) ya virusi vya
Varicella zoster virus kwa mama wajawazito kwa kuchukua maji kwenye chupa ya
uzazi ya mama (amniotic fluid). Kipimo hiki kina madhara kama kusababisha mimba
kutoka au mtoto kupata Fetal Varicella Syndrome
Matibabu
Matibabu ya ugonjwa huu yanalenga kupunguza athari za
dalili na viashiria vya ugonjwa huu na si kuua virusi vinavyosababisha ugonjwa
huu.
Matibabu ya tete kuwanga yanahusisha;
a) Kuwakata watoto kucha ili kuepusha kujikuna na hatimaye
kukata vipele hivyo kuongeza kutokea kwa vipele mwilini
b) Dawa za maumivu kama paracetamol n.k
c) Antihistamines-Dawa za kupunguza kuwashwa mwili
d) Calamine lotion ingawa hakuna tafiti zilizofanyika
kuthibitisha ubora wa matumizi yake dhidhi ya ugonjwa huu.Dawa hii ni salama
e) Kuongeza kiwango cha usafi wa mwili, kuosha mwili kwa
maji ya uvuguvugu
f) Kukaa sehemu zenye baridi ili kupunguza kuwashwa mwili
g) Kuepuka kujikuna vipele
h) Dawa dhidhi ya virusi (antiviral medication) kama
acyclovir au valacyclovir ambazo hutolewa saa 24-48 baada ya vipele kuanza,dawa
hizi hupunguza kusambaa kwa virusi lakini haziui virusi hao.Dawa hizi hutolewa
kwa wale ambao wana upungufu wa kinga mwilini na kwa wanawake wajawazito.Watoto
chini ya miaka 12 au wale wenye umri wa zaidi ya mwezi mmoja hawaruhusiwi
kutumia dawa hizi kama hawana tatizo la upungufu wa kinga mwilini ili
kuwaepusha na madhara wanayoweza kupata kutokana na matumizi ya madawa haya.
Madhara ya tete kuwanga kwa wajawazito
Maambukizi ya tete kuwanga wakati wa ujauzito yanaweza
kuathiri mtoto hasa kama mama atapata maambukizi haya wiki 28 baada ya kushika
mimba.Wanawake ambao wana kinga dhidhi ya ugonjwa huu hawawezi kupata tete
kuwanga kipindi cha ujauzito na wasiwe na wasiwasi kuhusu
mtoto wao kupata madhara.Madhara ya tete kuwanga kwa mtoto
ni kutokana na uwezo wa Varicella zoster virus kuwa na uwezo wa kuvuka kondo la
uzazi (placenta) kutoka kwa mama mwenye tete kuwanga na hivyo kumuathiri mtoto.
Maambukizi ya tete kuwanga kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto
kipindi cha ujauzito hujulikana kama fetal varicella syndrome au congenital
varicella syndrome na huambatana na;
I. Madhara kwenye ubongo wa mtoto-Kichwa maji (hydrocephalus),
kichwa kuwa kidogo, maambukizi ya ubongo (encephalitis),aplasia of brain
II. Madhara ya macho kama mtoto wa jicho (cataract), optic
cup, optic stalk,microphthalmia, cataracts, chorioretinitis, optic atrophy
n.k.
III. Madhara ya mishipa ya fahamu
IV. Madhara ya kibofu cha mkojo, miguu, njia ya haja
kubwa,vidole kutoota vizuri n.k.
V. Matatizo ya ngozi kama hypopigmentation na n.k.
Watoto wenye umri wa mwezi mmoja au watoto wachanga
wanatakiwa kulindwa wasipate tete kuwanga kwa kuweka mbali na wagonjwa wa tete
kuwanga kwa siku 10-21. Uwezekano wa mtoto kupata tete kuwanga ni mkubwa iwapo
mama atapata maambukizi ya tete kuwanga siku saba kabla ya kujifungua au wiki
moja baada ya mtoto kuzaliwa.


No comments