Leo
tuangalie tatizo la upungufu wa damu mwilini. Anaemia ni jina la jumla
linalotumiwa kubainisha aina mbalimbali za upungufu wa damu mwilini.
Kiwango cha kawaida cha chembe nyekundu za damu
(Haemoglobin-Hb) katika mwili wa binadamu ni kati ya gramu 12 mpaka 14
kwa kila mililita ya damu na zikiwa pungufu ya hapo mtu huyo anakuwa na
tatizo la upungufu wa damu.
Upungufu wa damu mwilini hutokea iwapo
mkusanyiko wa pamoja wa chembe nyekundu za damu zinapopungua kupita
kiwango cha kawaida kinachotakiwa kwenye mwili wa binadamu.
Tatizo hili linaweza kumpata mtu yeyote ingawa visababishi vinaweza kutofautiana.
Licha ya utofauti huo mara nyingi tatizo hili husababishwa na mambo makuu matatu ambayo ni kupoteza damu mfano wakati wa hedhi kwa wanawake hasa wanaotokwa na damu nyingi au kuvuja damu kunakosababishwa na vidonda vya tumbo.
Sababu nyingine ni uzalishwaji duni wa chembe
nyekundu za damu unaosababishwa na upungufu wa vitamini au lishe duni
pamoja na magonjwa sugu. Pia magonjwa ya kurithi.
Iwapo mtu atapungukiwa kiasi cha madini, ulaji
wa madini ya chuma katika mlo wa kawaida wa mtu hauwezi kufidia kiwango
cha madini kilichopotea na kiasi hicho kinachokuwa kimebaki hutumika
mara moja.
Aina za upungufu wa damu mwilini
Zipo aina mbalimbali za upungufu wa damu
ikiwemo Haemolytic Anaemia. Hali hii ya upungufu wa damu, chembe
nyekundu za damu huharibiwa haraka kuliko mwili unavyoweza kuzalisha
chembe nyingine.
Upungufu huu husababishwa na mambo mengi
ikiwemo kansa aina ya Lymphoma au utumiaji wa baadhi ya dawa ambazo
huweza kuangamiza chembe nyekundu za damu kwa mfano dawa aina ya
Methylodopa inayotibu matatizo ya presha ya kupanda.
Mtu mwenye aina hii ya upungufu wa damu anaweza kupatwa na homa, kutetemeka kwa mwili, maumivu ya tumbo na mgongo na mapigo ya moyo kushuka ghafla.
Pernicious Anaemia. Huu ni upungufu wa damu unaotokana na ukosefu wa kutosha wa asidi aina ya Folic (Folate) katika chakula.
Asidi aina ya Folate hupatikana katika
mbogamboga za rangi ya kijani, matunda na nyama.Aplastica Anaemia. Huu
ni upungufu wa damu unaotokea wakati chembe nyekundu za damu
zinaposhindwa kuzalishwa ipasavyo.
Sickle cell Anaemia. Ni aina nyingine ya
upungufu wa damu ambao chembe nyekundu za damu huwa na muundo usio wa
kawaida unaozuia na kuathiri mishipa midogo ya damu na hivyo kusababisha
kuziba kwa mishipa hiyo ya damu.
Dalili za upungufu wa damu mwilini (anaemia)
Mtu mwenye tatizo la upungufu wa damu mara
nyingi huwa amepauka mwili na hujisikia kuchoka, udhaifu na huwa na
mwendo kasi wa damu (yaani high pulse rate). Mgonjwa kuhisi kiu,
kizunguzungu wakati akisimama, moyo kwenda kasi wakati akitumia nguvu
kufanya jambo lolote, kuhema mfululizo na kupumua haraka haraka.
Dalili nyingine ni mapigo ya moyo kwenda kwa
kasi, kuhisi uchovu sana au hata kuishiwa kabisa na nguvu. Wakati
mwingine mgonjwa anaweza kuhisi maumivu ya kifua pamoja na
kuchanganyikiwa anaposhughulikia jambo fulani.
Kuvimba kwa tumbo au sehemu za chini yake,
kupoteza nguvu na macho kukosa nuru ya kuona vizuri ni dalili nyingine
za mtu mwenye tatizo hili.
MATIBABU YAKE
Matibabu ya upungufu wa damu aina yoyote yanategemea aina ya upungufu wa damu inayomkabili mgonjwa.
Upungufu wa damu hutibiwa mapema kwa kubadili
lishe pamoja na kuongeza lishe yenye vitamini C na B12 pamoja na madini
ya chuma kutokana na visababishi vya tatizo.
Matibabu ya lishe yanaweza kutumika kwa ushauri wa daktari ingawa yanaweza yasitoshe hadi pale mgonjwa atakapoongezewa damu.
Mara nyingine vidonge na sindano zenye lishe
hizo huweza kutumiwa na madaktari hospitalini sambamba na matibabu ya
tatizo linalosababisha na iwapo mgonjwa yuko mahututi huweza kuongezewa
damu. Ushauri, ukiona dalili hizo, muone daktari haraka
No comments