TATIZO LA KUZIBA KWA MIRIJA YA UZAZI (FALLOPIAN TUBES)

 

Mirija ya uzazi kitaalamu inajulikana kama Fallopian tubes. Hii ni mirija midogo iliyopo kwenye mfumo wa uzazi wa mwanamke ambayo husaidia kupitisha yai lililopevuka hadi kufika kwenye mji wa mimba.

Mirija hii inapoziba inazuia yai kusafiri baada ya kuachiliwa na mfuko wa mayai pia inazuia mbegu za kiume kulifikia yai.Tatizo hili ni moja kati ya sababu za ugumba kwa wanawake. ambapo Asilimia 40 ya wanawake wenye matatizo ya ugumba inasababishwa na tatizo la mirija kuziba.
Mara nyingi wanawake wenye tatizo hili hua hawaoneshi dalili zozote zile.

KUZIBA KWA MIRIJA YA UZAZI KUNASABABISHA VIPI UGUMBA?
Kila mwezi yai la  mwanamke linapopevuka huachiliwa kutoka kwenye mfuko wa mayai na kusafiri kupitia mirija ya uzazi kuelekea kwenye mji wa mimba. Mbegu za kiume pia husafiri kutokea kwenye shingo ya kizazi na kulifata yai kwenye mirija ya uzazi ili kulirutubisha. tuelewe kwamba urutubishwaji wa yai unafanyika kwenye mirija ya uzazi wakati yai linasafiri kuelekea kwenye mji wa mimba.
Mirija inapokuwa imeziba inzauia yai kusafiri kufika kwenye mji wa mimba na inazuia mbegu za kiume kulifikia yai hivyo kusababisha ugumba.

Mbali na hayo mirija hii inaweza isizibe yote kabisa na kuacha upenyo unaoruhusu mbegu za kiume kupita na kulifikia yai na kupelekea mimba kutunga nje ya kizazi.

DALILI ZA MIRIJA YA UZAZI KUZIBA
Sio watu wote wenye tatizo hili huonesha dalili.Asilimia kubwa ya wanawake wenye tatizo hili hawaoneshi dalili zozote.
Aina ya tatizo hili inayojulikana kitaalamu kama HYDROSALPINX ndo huwa na dalili za maumivu ya tumbo chini ya kitovu na kutokwa na maji maji mengi ukeni.
Hydrosalpinx ni aina ya tatizo la mirija kuziba ambapo mirija inaziba na kujaa maji.
pia mwanamke huweza kupata dalili kama maumivu makali wakati wa tendo la ndoa na maumivu makali wakati wa hedhi

VISABABISHI VYA TATIZO LA MIRIJA KUZIBA
Kisababishi kikubwa cha mirija kuziba ni tatizo la maambukizi kwenye viungo vya uzazi (PID)
Na mara nyingi PID husababishwa na maambukizi ya magonjwa ya zinaa japo sio kila mwenye PID imetokana na magonjwa ya zinaa.

Sababu nyingine ni kama
Magonjwa ya zinaa mfano Kisonono na Chylamidia
Maambukizi kwenye kizazi baada ya mimba kuharibika (abortions)
Historia ya tatizo la kidole tumbo (Appendicitis)
Historia ya Mimba kutunga nje ya kizazi
upasuaji ambao unahusisha mirija ya uzazi

VIPIMO GANI VYA KUONESHA TATIZO HILI?
Tatizo hili upimwa kwa kipimo maalumu cha X ray ambacho kinajulikana kitaalamu kama Hysterosalpingogram (HSG) ambapo unawekewa kimiminika fulani ambacho ni salama kwenye kizazi na kupigwa X ray. Kimiminika hicho kikiingia kwenye kizazi kinaenda hadi kwenye mirija kikishndwa kupita kwenye mirija basi inaonesha mirija imeziba.Aina nyingine ya kipimo hiki ni kwa kuwekewa kifaa chenye camera ambacho kinapitishwa ukeni hadi kwenye mirija. Vipimo vingine ni vile vya kupima ute (High vaginal swab) kuangalia kama kuna maambukizi.

MATIBABU
Kama mirija imeziba kwa makovu madogo madogo basi huzibuliwa kwa vifaa maalumu au upasuaji wa kutoa makovu hayo.
Endapo mirija imeziba kwa kujaa maji kwa sababu ya maambukizi (hydrosalpinx) basi unahitaji matibabu ya maambukizi hayo kwanza.

UWEZEKANO WA KUPATA UJAUZITO
Mirija ikishazibuliwa unaweza kushika mimba kawaida. kama una matatizo ya kupevusha mayai daktari anaweza kukuongezea dawa za kusaidia kupevusha mayai.

Endapo mirija imeziba hata unapotumia dawa za kupevusha mayai haziwezi kukusaidia.

Mwisho
Ni vyema unapofikilia kupata ujauzito ufanye vipimo vinavyosaidia pia kuona mirija yako kama iko katika hali nzuri.Unapoona dalili zozote ambazo huzielewi kwenye mwili wako basi hakikisha unafika hospitali kwa ajili ya matibabu


No comments