Kwa kuwa na kizunguzungu kunaweza kukaathiri shughuli zako za kila siku. Lakini pia ni mara chache sana kizunguzungu kikawa ni dalili za tatizo linalo hatarisha maisha.
- Kuhisi kama kichwa au mwili mzima unazunguuka
- Hali ya kujisikia kama unataka kupoteza fahamu au kichwa kuwa chepesi
- Kukosa balance
- Kuhisi kama unaelea angani au kwenye maji
Dalili hizi zinaweza kuanza mara baada ya mtu aliyekuwa amekaa akaamka kiasi cha kumfanya atulie kwanza kabla ya kuanza kutembea, au aliyesimama anapotembea, au kugeuza kichwa. Hali ya kizungunguzu mara nyingi huambatana na kichefuchefu. Kizunguzungu kinaweza kudumu kwa sekunde au hata wiki kadhaa na kinaweza kujirudia rudia baadae baada ya kutulia kwa muda fulani
Sababu za kwenda hospitali
Inashauriwa kumuona daktari utakapoona dalili zinajirudia rudia, au unapopata kizunguzungu ambacho ni cha ghafla na kikadumu kwa muda mrefu. Pia kikiambatana na dalili zifuatazo:
- Maumivu makali ya kichwa
- Maumivu ya kifua
- Kupumua kwa shida
- Ganzi ya ghafla au kupooza kwa miguu, mikono au usoni
- Kupoteza fahamu
- Kuona maruweruwe (double double)
- Mapigo ya moyo kwenda mbio na au kupiga ovyo ovyo bila mpangilio
- Kuchanganyikiwa au kuongea kwa shida
- Kutapika kusikokoma
- Kujikwaa kwaa bila sababu au kutembea kwa shida
- Degedege
- Kutosikia vyema kwa ghafla
Ziko sababu kadha wa kadha zinazoleta kizunguzungu kama matatizo ya masikio, athari za kusafiri, dawa, magonjwa kama Malaria, magonjwa ya moyo, shinikizo la damu, Kisukari, na ajali. Jinsi kizunguzungu kinavyokufanya ujisikie au mambo yanayofanya kianze au muda kinaokuwepo na dalili zingine zinazoambatana nazo, vyote hivyo hutoa mwanga kwa daktari kujua chanzo.
Matatizo ya viuongo vya ndani vya sikio.
Uwiano (balance) anaokuwa nao mtu aliye mzima na kumwezesha kutembea bila kupepesuka unatoka na kazi ya viungo mbalimbali vya hisia vya mwili wa binadamu. Viungo hivi ni:
- Macho, kazi yake ni kukuwezesha kujua uko wapi na unatembeaje au kosogea.
- Mishipa ya fahamu, kazi yake ni kupeleka taarifa kwenye ubongo kuhusu mwendo na mwili ulipo
- Sehemu ya ndani ya sikio, Sikio lina sehemu kuu tatu, sehemu ya nje ambayo tunaiona kwa urahisi, sehemu ya kati ilipo ngoma ya sikio, na sehemu ya ndani kabisa ya sikio ambayo ni baada ya ngoma, hii huwa hatuioni kwa macho. Sehemu ya ndani kabisa ya sikio ina viuongo ambavyo vinatusaidia kupata uwiano (balance) wa mwili kwa kusaidiana na viungo vingine nilivyovitaja hapo juu. Husaidia kujua nguvu za uvutano (gravity) na kukufanya ujue kama unaenda mbele au unarudi nyuma.
- Kizunguzungu kisichofahamika chanzo (Benign Paroxysmal Positional Vertigo) – Kizunguzungu hiki hakina athari kubwa kwa maisha ya muhusika. Aina hii ya kizunguzungu hakifahamiki chanzo chake (idiopathic), kwa lugha nyepesi tungesema cha kuzaliwa nacho. Hutokea pale mtu anapobadili mkao ghafla; kuamka na kukaa kitandani ghafla au kusimama ghafla kwa mtu aliyekuwa ameketi. Pia kugeuza au kuinamisha au kuangalia juu haraka.
- Uambukizo; Mishipa ya fahamu ya sehemu ya ndani ya sikio inapopata uambukizo wa aina fulani ya virusi na kusababisha kizunguzungu na wakati mwingine hata kutosikia sawa sawa.
- Kujaa kwa majimaji sehemu ya ndani ya sikio (Meniere’s disease); hapa tunamaanisha maji yanayotengenezwa ndani ya sikio kwasababu fulani fulani huzidi kiwango kinachokubalika na kusababisha kizunguzungu ambacho hudumu kwa masaa kadhaa. Pia huleta kuziba na kuzibuka kwa masikio, sauti za kengele na kuhisi kama vile sikio limezibwa kwa pamba.
- Kipanda uso (Migraine). Watu wanaopata matatizo ya kipanda uso hupata pia kizunguzungu hata kama kwa wakati huo kichwa hakiumi. Kizunguzungu wanachopata hawa huwa kina dumu kwa dakika hadi saa kadhaa na kupotea. Pia wanakuwa na hali ya kutotaka makelele, sauti ndogo wao huhisi ni kelele kubwa sana.
Matatizo ya mzunguuko wa damu unavyoweza kuleta Kizunguzungu
- Kushuka kwa shinikizo la damu (Low Pressure). Kushuka kwa ghafla kwa shinikizo la damu kunaleta kizunguzungu cha muda mfupi. Hali hii inaweza kutokea iwapo utasimama ghafla kama ulikuwa umeketi au kuamka na kuketi kitandani ghafla. Kubadilika kwa mkao wa mwili huku kunasababisha shinikizo la damu lishuke ghafla kwani mwili unakuwa haujapata muda wa kujiweka sawa.
- Matatizo ya kutozunguuka vyema kwa damu; huku kunatokea kwa watu wenye magonjwa ya moyo kuwa mkubwa (Cardiomyopathy), shambulio la moyo (Heart attack), na mapigo ya moyo yaliyoparaganyika (Arrhythmia). Matatizo haya yote yanababisha moyo ambao ndiyo pump, kupungua uwezo wa kusukuma damu ya kutosha kwa ajili ya mahitaji ya mwili, ikiwemo ubongo na sehemu ya ndani ya sikio.
Sababu zingine zinazoleta kizunguzungu
- Magonjwa ya mishipa ya fahamu
- Dawa zinazotumika kutibia matatizo mbalimbali yanaweza kuwa chanzo cha kizunguzungu. Mfano dawa za kuzuia degedege, dawa za sonona, na dawa za kutibu shinikizo la damu pia huwa ni sababu kwani kuna wakati hushusha shinikizo la damu kufikia chini ya kiwango.
- Aina fulani ya magonjwa yanayomfanya mtu kuwa na wasiwasi kuliko kawaida huleta kizungunguzu.
- Upungufu wa damu. Kupungua kwa wekundu wa chembechembe nyekundu za damu huleta kizungunguzu kwani kiwango cha hewa ya oxygen kinachozunguuka kinakuwa kidogo.
- Kushuka kwa sukari. Hali hii huwapata watu wenye kisukari wanaotumia insulin ambayo inaweza kusababisha sukari kushuka sana. Pia hata wenye njaa kupita kiasi.
- Joto kali na kupungukiwa maji. Joto kali husababisha kutokwa na jasho jingi hivyo maji mwilini kupungua na kuleta kizunguzungu.
Athari
Athari kubwa za kizunguzungu zinakuja pale ambapo kizunguzungu kinapoweza kusababisha muhusika kuanguka chini. Kitendo cha kuanguka kinaweza kuleta majeraha mbalimbali mwili kulingana na namna na mahala alipoangukia muhusika. Athari nyingine ni za kiuchumi na kijamii pale ambapo kizunguzungu kikiwa cha muda mrefu na kusababisha muhusika ashindwe kushiriki shughuli za kumuingizia kipato na za kijamii.
Utambuzi
Utambuzi wa matatizo yanayoleta kizunguzungu yatahusisha uchukuaji wa maelezo na kufanya vipimo ambavyo daktari ataona vinafaa.
Matibabu
Yatategemeana na chanzo kilichogundulika. Matibabu yanaweza kuhusisha dawa, upasuaji na mazoezi.
No comments