Ikumbukwe kuwa, watoto wanaotumia waziwa mbadala (formular) wao hunywa mara chache zaidi ya wale wanaonyonya maziwa ya mama kwa sababu, maziwa ya mama humeng'enywa kwa urahisi zaidi kuliko yale ya unga (ng'ombe). Ikumbukwe pia, jinsi unavyomnyonyesha mtoto, ndivyo mwili wako unavyotengeneza maziwa zaidi, hii husaidia sana kwa wamama wenye matatizo ya utoaji maziwa ya kutosha.
Hebu tuangalie mahitaji ya maziwa kwa kila kipindi.
Siku za kwanza
Siku za mwanzo za maisha baada ya kuzaliwa, tumbo la mtoto huwa dogo sana, hivyo hahitaji maziwa mengi. Unashauriwa kumnyonyesha kila baada ya saa 1 hadi 3. Katika kipindi hiki, utajua kama mtoto anaendelea kuhitaji kama anaendelea kuvuta na kumeza. Epuka kumuacha mtoto akiwa na maziwa mengi mdomoni kwani inaweza kupelekea kupaliwa. Maziwa ya Mama ni muhimu sana katika siku hizi za mwanzo hivyo jitahidi na hakikisha anapata maziwa ya kutosha.
Wiki za na Miezi ya mwanzo
Kadri mtoto anavyokua, basi tumbo na viungo vyake vinakua vikubwa na kuwa tayari kiutendaji. Kadri siku zinavyoenda, mtoto anakuwa yupo tayari kunyonya zaidi. Jinsi mtoto anvyoendelea kukua, kwakuwa huwa na uwezo wa kunyonya kiasi kikubwa kwa wakati, basi, muda wa kumnyonyesha hupishana kuanzia masaa 2 hadi 4 tofauti na ilivyokuwa siku za awali. Kumbuka, wakati huu, mtoto hutumia muda mwingi kulala, hivyo inawezekana kabisa muda wake wa kunyonya ukapitiliza.
Ikumbukwe pia, hakuna muda rasmi wa kumnyonyesha mtoto, kwani kuna wakati naweza kunyonya kwa muda mrefu na kuna wakati anaweza kunyonya kwa muda mchache kutegemeana na mahitaji yake. Mara nyingi, watoto hunyonya kulingana na mahtaji na huacha pale wanapoona hawahitaji tena. Katika kipindi hiki, mtoto anaweza kunyonya mara 8 hadi 12 ndani ya masaa 24.
Miezi 6 hadi mwaka mmoja
Kwakuwa kuanzia miezi 6 mtoto anakuwa ameshaanza kutumia vyakula vingine, hivyo muda wa unyonyaji hupishana sana kutoka mtoto mmoja hadi mwingine. Kitu muhimu cha kuzingatia ni kumsoma na kufuatilia mahitaji ya mtoto pale anapohitaji kunyonya au anapokuwa na njaa. Kuna baadhi ya watoto huacha kupendelea kunyonya baada ya kuanza kula vyakula, hivyo kama hali hii itajitokeza kwa mtoto wako, inashauriwa umnyonyeshe kwanza kabla ya kuanza kumpa chakula kingine.
Kumbuka kuwa, hata kama mtoto tayari ameshaanza kutumia vyakula vingine, bado maziwa ya mama tegemeo kuu la virutubisho kwa mtoto katika umri huu, hivyo usiache kuendelea kumnyonyesha hata kama anakula vizuri vyakula vingine.
Miezi 12 hadi 24
Kwa kipindi hiki, mahitaji nayo hutofautiana sana kutoka mtoto mmoja hadi mwingine. Kuna watoto hupendelea kunyonya asubuhi na jioni tuu wakati wengine huendelea kunyonya mara nyingi katikati ya siku au kupishana na mlo wao. Kitu cha msingi ni kumfuatilia na kujua mahitaji ya mtoto bila kumlazimisha au kumpunja.
Utajuaje kama mtoto anahitaji kunyonya?
Inashauriwa Mama kumnyonyesha mtoto pale anapohisi kuwa ana njaa. Wengi wamekuwa wakitegemea kumsikia mtoto analia kama ishara ya njaa, lakini kulia ni ishara ya mwisho ya njaa, ina maana mpaka analia itakuwa ameshasikia njaa na ameshindwa kuvumilia. Pia, kulia haimaanishi kuwa ana njaa,
Zifuatazo ni baadhi ya ishara kuwa mtoto ana njaa;
- anazungusha kichwa huku na huku
- anaachama mdogo
- anang'atang'ata ulimi kama anamung'unya kitu
- anakula vidole
- analamba midomo
- anajalibu kushikashika
Ninajuaje kama toto hapati maziwa ya kutosha?
Swali hili ni moja ya maswali ambayo wamama wengi wamekuwa wakijiliza, je nitajuaje kama mtoto anapata maziwa ya kutosha. Zifuatazo ni baadhi ya ishara kuonesha kuwa mtoto hapati mawiwa ya kutosha
- Unamuona anakuwa hajatosheka hata baada ya kunyonya
- anakuwa na njaa kwa vipindi vifupivifupi sana
- anapata choo au mkojo mara chache saaana
- ana hasira na ana lialia sana
- haongezeki uzito


No comments