TATIZO LA MDOMO SUNGURA`



Mdomo sungura (cleft lip and  palate) ni aina ya ulemavu unaosababishwa na sehemu ya uso na mdomo kushindwa kufungwa mtoto anapokuwa akitengenezwa akiwa tumboni. Tatizo la mdomo sungura ni tatizo linalowapata watoto wengi katika jamii. Hali hii hutokea katika wiki ya tano hadi ya nane ya ukuaji wa mtoto anapokua tumboni ambapo sehemu tatu za uso yaani sehemu ya juu, pembeni na chini hushindwa kukutana.

Visababishi vya mdomo sungura.

Kuna visababishi mbalimbali vinavyopelekea mtoto kuzaliwa na ulemavu wa mdomo sungura. Kwa mujibu wa uchunguzi uliofanyika na wataalamu mbalimbali hali hii husababishwa na muingiliano wa matatizo ya vinasaba na sababu za kimazingira kama;
  • Sababu isiojulikana (idiopathic reason)
  • Unywaji wa pombe uliokithiri kipindi cha ujauzito.
  • Uvutaji wa tumbaku kipindi cha ujauzito.
  • Lishe duni kwa mama mjamzito, kama kukosa virutubisho muhimu kama vile vitamini aina ya asidi ya foliki.
  • Matumizi ya baadhi ya dawa kama dawa za degedege haswa katika kipindi cha ujauzito.

Aina za mdomo sungura.


Mdomo sungura ulioathiri sehemu ya mdomo na pua. Aina hii ya mdomo sungura huathiri sehemu ya mdomo na pua zaidi.
Aina ya pili ya mdomo sungura  ni ile inayo athiri sehemu ya juu ndani ya mdomo. Sehemu hii huwa na  uwazi.
Aina ya tatu huambatanisha aina zote mbili za mwanzo. Aina hii huathiri sehemu zote, yani sehemu ya nje ya mdomo, pua na ndani ya mdomo unakua na uwazi.

Tiba kwa mtoto mwenye ulemavu wa mdomo sungura

Ulemavu wa mdomo sungura una tiba. Watoto wenye ulemavu huu hufanyiwa upasuaji na kurudisha viungo vyao vilivo athirika katika hali iliyo ya kawaida. Upasuaji huu hufanywa na wataalamu waliopo katika hospitali mbalimbali hapa nchini.

Kinga dhidi ya mdomo sungura kwa mtoto.

Tatizo hili la ulemavu wa mdomo sungura huwapata watoto. Lakini kinga ya ugonjwa huu huanzia kwa mama haswa katika kipindi anapokua mjamzito. Zifuatazo ni kinga dhidi ya mdomo sungura ambazo mama anatakiwa kupata pindi anapokua mjamzito;
  • Uzuiaji wa unywaji wa pombe.
  • Dhibiti uvutaji wa sigara.
  • Lishe yenye virutubisho vyote kwa mama mjamzito.
  • chanjo ya vitamini ya aina ya asidi ya foliki.

No comments