SARATANI YA TEZI YA THYROID (THYROID CANCER)
Hii
ni aina ya saratani inayokumba tezi ya thyroid. Ikumbukwe kuwa tezi ya
thyroid ipo sehemu ya mbele ya shingo ya mwanadamu ikiwa na sehemu mbili
(lobes) moja kila upande wa shingo.
Visababishi na ukubwa tatizo
Saratani
ya thyroid huwapata watu wa umri mbalimbali, kuanzia watoto mpaka watu
wazima. Watu waliowahi kupigwa mionzi sehemu ya mbele ya shingo wapo
katika hatari kubwa ya kupata aina hii ya saratani. Kadhalika watu
wazima ambao waliwahi kupigwa mionzi kipindi cha utotoni nao pia wana
hatari kubwa zaidi ya kupata saratani ya thyroid hata kama hawakuwahi
kupata tatizo hilo wakati wanakua.
Tiba ya mionzi maeneo ya
shingoni ilikuwa ikitumika sana zamani kwenye miaka ya 50 mpaka 60 kwa
ajili ya matibabu ya uvimbe wa tezi ya thymus, mafindofindo (tonsils),
au baadhi ya magonjwa ya ngozi. Hata hivyo ni nadra sana kwa tiba hii
kutumika katika zama hizi.
Vihatarishi vingine vya saratani ya tezi
ya thyroid ni pamoja na kuwepo kwa historia ya tatizo hili miongoni mwa
wanafamilia na kuwa na goita iliyodumu muda mrefu bila kutibiwa.
Aina za saratani ya tezi ya thyroid

Kulingana
na aina ya seli zinazounda tezi ya thyroid zinazoshambuliwa, saratani
ya thyroid inaweza kugawanywa katika aina zifuatazo:
• Aina
inayojulikana kitaalamu kama papillary carcinoma. Hii ni aina maarufu
zaidi miongoni mwa watu wenye saratani ya tezi ya thyroid. Kwa kawaida,
aina hii huwapata zaidi wanawake walio katika umri wa kuzaa. Aina hii
husambaa taratibu sana na haina madhara sana kwa mgonjwa ikilinganishwa
na aina nyingine za saratani ya tezi ya thyroid.
• Aina nyingine ni
ile inayofahamika kwa jina la follicular carcinoma. Aina hii hutokea
katika asilimia karibu 10 ya watu wanaopata saratani ya thyroid.
Follicular carncinoma huwa na tabia ya kupotea lakini pia huwa na uwezo
wa kumrudia mgonjwa na kisha kusambaa kwa kasi.
• Aina ya tatu ni ile
inayojulikana kama anaplastic carcinoma. Aina hii, japokuwa ni nadra
sana kuonekana miongoni mwa wagonjwa wenye saratani ya thyroid, ndiyo
aina ya hatari zaidi miongoni mwa aina zote za saratani ya thyroid.
Anaplastic carcinoma husambaa kwa kasi kubwa na haiwezi kutibika kwa
kutumia tiba ya madini ya nuklia ya Iodine.
• Aina nyingine huitwa
medullary carcinoma. Hii ni aina ya saratani ya thyroid ambayo hutokea
katika seli ambazo si za tezi ya thyroid lakini zipo ndani ya tezi hiyo
(kuna baadhi ya seli ambazo si za tezi ya thyroid lakini zinapatikana na
kuishi ndani ya tezi ya thyroid, mfano wa mgeni anayeishi katika nyumba
isiyo yake). Aina hii huwapata zaidi wanafamilia na watafiti
wameihusisha na mabadiliko ya kinasaba (genetic mutations), na kwa
ujumla matibabu yake hutofautiana sana na yale ya aina nyingine za
saratani ya thyroid.
Dalili
Dalili hutofautiana kulingana na aina ya saratani, ingawa kiujumla zaweza kujumuisha:
• kikohozi
• Shida wakati wa kumeza chakula, vinywaji hata mate
• Kuvimba kwa tezi ya thyroid
• Mabadiliko katika sauti, sauti kufifia au kuwa ya mikwaruzo
• Uvimbe kwenye shingo
• Tezi ya thyroid kuwa na nundu au vinundu
Vipimo na uchunguzi
Mgonjwa
anayehisiwa kuwa na saratani ya thyroid hufanyiwa uchunguzi wa mwili
kabla ya kufanyiwa vipimo kadhaa ili kujiridhisha kuwa ni kweli ana
tatizo la saratani ya thyroid. Uchunguzi wa mwili unaweza kuonesha uwepo
wa nundu au uvimbe katika thyroid na/ kuvimba kwa tezi za mitoki katika
shingo.
Vipimo ni pamoja na:
• Ultrasound ya tezi ya thyroid
• Kukata sehemu ya thyroid na kukichunguza kimaabara (thyroid biopsy)
• Picha ya utendaji kazi wa tezi ya thyroid (thyroid scan)
• Uchunguzi wa sehemu ya ndani ya koo (laryngoscopy)
•
Kupima damu ili kuchunguza kiwango cha homoni ya calcitonin. Iwapo
kiwango kitakuwa juu kuliko kawaida, hii yaweza kuashiria uwepo wa
medullary carcinoma.
• Kupima damu ili kuchunguza kiwango cha viasili
vya thyroglobulin ambavyo vywaweza kuashiria uwepo wa saratani aina ya
papillary carcinoma au follicular carcinoma.
• Kupima damu ili kuchunguza kiwango cha homoni za thyroid za T3, T4 na TSH.
Matibabu
Matibabu
hutegemea sana aina ya saratani, ingawa upasuaji wa tezi ya thyroid
ndiyo aina ya tiba inayoongoza. Wakati wa upasuji, kwa kawaida tezi yote
huondolewa, na iwapo daktari atahisi kuwa hata tezi za mitoki zilizo
karibu na thyroid nazo pia zimeathirika pia huondolewa.
Aidha
mgonjwa anaweza pia kupatiwa tiba ya mionzi ambayo hutolewa kwa njia ya
kupigwa mionzi ya moja kwa moja (external beam radiation) au kwa kutumia
(kunywa) vidonge vya madini ya Iodine vyenye nguvu ya nyuklia yaani
radioactive iodine. Njia hii inaweza kufanyika ikiambatana pia na
upasuaji au bila upasuaji.
Baada ya matibabu, mgonjwa anapaswa
kuendelea kutumia dawa maalum za kumrejeshea homoni za thyroid ili
kurudisha kile alichopoteza baada ya kuondolewa kwa tezi. Kwa kawaida
dozi inayotolewa huwa kubwa kuliko ile inayohitajika mwilini ili
kusaidia saratani isijirudie tena.
Iwapo upasuaji au mionzi
haujasaidia kuondoa kansa, na kwamba saratani inaendelea kusamabaa
sehemu nyingine za mwili, mgonjwa anaweza kuanishiwa dawa za kutibu
saratani (chemotherapy) ingawa nayo inaweza ikawa na manufaa kwa baadhi
ya wagonjwa tu na si wagonjwa wote.
Nini cha kutarajia
Saratani
aina ya Anaplastic carcinoma ina matokeo mabaya zaidi kuliko aina zote
zilizobaki, na mara nyingi mgonjwa hufariki hata baada ya matibabu ya
uhakika ya muda mrefu. Follicular carcinomas pamoja na kuwa na tabia ya
kusambaa kwa kasi
kwenye maeneo mengine ya mwili huwa na matokeo
mazuri ikitibiwa. Matokeo ya wagonjwa wenye aina ya medullary carcinoma
yanatofautiana kati ya mgonjwa na mgonjwa, ambapo wanawake wenye umri
chini ya miaka 40 wameonekana kuwa na matokeo mazuri zaidi baada ya tiba
kuliko walio na zaidi ya umri huo. Aidha wagonjwa wengi wenye Papillary
carcinomas hupona kabisa na kuendelea na maisha yao ya kawaida.
Jambo
la kukumbuka ni kuwa, mara baada ya tiba, mgonjwa anapaswa kuendelea
kutumia vidonge vya kurejesha homoni za thyroid kila siku za maisha
yake.
Madhara ya saratani ya thyroid
Madhara ya saratani ya
thyroid ni pamoja na madhara katika sanduku la sauti kabla ya upasuaji,
na sauti ya mikwaruzo baada ya upasuaji, kupungua kwa kiwango cha madini
ya calcium mwilini iwapo tezi ya parathyroid ambayo ipo juu kidogo ya
thyroid itaodolewa kwa bahati mbaya wakati wa upasuaji, na kusambaa kwa
kansa katika sehemu nyingine za mwili kama vile mifupa, au mapafu.
No comments
Post a Comment