Katika
maisha ya kila siku ya mwanadamu, swala la kuugua au kupata ugonjwa ni
la kawaida, ni kawaida kwa sababu vijidudu vinavyosababisha magonjwa
vimetapakaa katika mazingira yetu, na hii ni katika hewa tunayoivuta,
maji tunayotumia na pia katika ardhi. Mbali na vijidudu pia yapo baadhi
ya magonjwa ambayo humpata mtu pengine kwa njia ya kurithi au kutokana
na aina ya maisha anayoishi (life style).
Jambo muhimu katika kukabiliana na matatizo haya ya kiafya ni kuzingatia ushauri kutoka kwa wataalamu wa afya.
Kwanza utakubaliana na mimi kuwa, tunakula chakula ili tuweze kuishi, hivyo basi, njia mojawapo ya mtu kuweza kupambana na magonjwa mbalimbali ni kula chakula ambacho ni salama kwa afya yake, chakula kinachoujenga mwili, kinachoupa nguvu na kuupa mwili uwezo wa kujilinda dhidi ya magonjwa mbalimbali na hivyo kukuwezesha kuishi huku ukiwa na afya bora.
Lakini inawezekana kwa bahati mbaya ukaugua, pamoja na utumiaji wa chakula na vinywaji ili kuimarisha hali ya afya yako, je dawa unazitumiaje?.
Katika
utumiaji wa dawa ili kuuwezesha mwili kupambana na magonjwa na pia kuupa
uwezo wa kufanya kazi vizuri, wengi wetu tumekuwa tunatumia dawa kwa
mazoea, katika hili namaanisha inawezekana mtu akatumia dawa kwa tatizo
ambalo halihitaji atumie dawa, mfano mwili umechoka kwa kuwa umefanya
kazi nzito na unahitaji kupumzika, ila kwa kuwa ni mazoea mtu anaona
bora atumie dawa ya maumivu, au wengine tunatumia dawa kwa kuwa
rafiki/ndugu yetu aliwahi kutumia dawa ya aina hiyo, bila kujua kama
dawa hiyo inakufaa pia wewe, au wengine tunatumia dawa kwa kuwa
tumejipima kwa macho/uelewa wetu na kujipatia tatizo fulani na kuamua
kujipangia dawa ya tatizo hilo, au wakati mwingine tunaamua kutumia dawa
katika dose tunazotaka sisi ili tuweze kutumia chakula/kinywaji fulani
ambacho hakitakiwi kutumiwa wakati unaendelea na dose ya dawa. Haya ni
baadhi ya mazoea tuliyonayo katika utumiaji wa dawa ambayo siyo mazuri.

Matatizo yanayosababishwa na utumiaji mbaya wa dawa ni kama vile, vidonda vya tumbo (utumiaji mbaya wa dawa za maumivu), dawa kushindwa kutibu ugonjwa (Drug Resistance) pamoja na vifo.
Unapopatwa
na tatizo la kiafya, chukua muda kujiridhisha katika mambo kadhaa
mfano, kupima afya ili kujua ni nini kinakusumbua, hakikisha umepata
maelekezo ya kutosha kutoka kwa mtaalamu wa afya juu ya aina ya dawa
unayopaswa kutumia, dose yake, urefu wa muda unaopaswa kutumia dawa na
pia shauriana na mtaalamu wa afya kujua ni wakati gani unaofaa zaidi
kwako wewe kutumia dawa.
Ili tuweze kuwa na afya bora ni vyema tukala chakula bora, tukanywa vinywaji salama na ikitokea ukaugua basi ni bora zaidi ukafuata ushauri wa mtaalamu wa afya ili kupunguza matatizo tunayoyapata kwa utumiaji mbaya wa dawa.


No comments