SARATANI
au kitaalamu Cancer ni moja ya magonjwa yanayowashambulia binadamu.Kuna
aina nyingi ya saratani kama vile ile ya matiti (breast) , mifupa
(bones) ubongo (brain), damu (Leokamia) na kadhalika.
Tutazungumzia mfululizo wa magonjwa ya saratani hizo na leo tutajadili
saratani ya mapafu, ugonjwa ambao ni hatari sana kwa binadamu.
DALILI YA SARATANI YA MAPAFU
Kuna dalili nyingi za mtu ambaye amekumbwa na ugonjwa huu, moja ya dalili ya wazi ni kupatwa na kikohozi mara kwa mara.
Baadaye mtu huyo ambaye anakohoa atapata tatizo la kushindwa kupumua
kwani atakuwa akifanya hivyo kwa taabu sana. Ugonjwa huu usipogundulika
mapema husambaa katika tezi ambazo zipo karibu na mapafu hivyo mgonjwa
kusikia maumivu makali.
Saratani hii ya mapafu pia inaweza kusambaa mpaka katika tishu nyingine
kama vile kwenye ngozi laini ya mapafu na katika moyo hivyo kuzidisha
hatari kwa maisha ya mtu anayeugua maradhi haya.
Baadhi ya wagonjwa wa saratani hii ya mapafu huweza kuwasababishia matatizo katika ubongo wao, hivyo kujisikia kuumwa na kichwa.
Maradhi haya baadaye huenda katika ini hivyo kumtia matatizo mgonjwa na kwa hakika hali ikifikia hivyo huwa ni hatari.
Saratani ya mapafu huwa ndiyo chanzo kikuu cha mtu kupatwa na saratani ya mifupa ikienea sehemu zote mwilini.
NINI HUSABABISHA KUUGUA MARADHI HAYA
Zipo sababu nyingi za mtu kuugua saratani ya mapafu lakini uvutaji wa
sigara, bangi au dawa za kulevya ni moja ya njia ya kusababisha mtu
kuugua maradhi haya japokuwa kuna baadhi ya watu huwa wanarithi ugonjwa
huu.
VIPIMO
Vipimo vya kubaini kama mtu ana saratani ya mapafu au la vipo vingi,
daktari anaweza kuamua kutumia kipimo kiitwacho kitaalamu CT au kipimo
kingine kiitwacho X – rey ambapo mgonjwa atapigwa picha na chombo hicho
sehemu ya kifuani.
Uchunguzi huo utaweza kumfanya daktari kugundua kama saratani hiyo ya
mapafu ipo katika pafu moja au mapafu yote na ataweza kujua kama mgonjwa
ana seli zisizo ndogo au seli ndogo na atajua kama ugonjwa huo umeenea
sana mwilini au la!
TIBA
Tiba ya saratani hii hutegemea uchunguzi ambao utagundua ni kwa kiasi
gani mtu ameathirika, daktari anaweza kuamua kufanya upasuaji au kwa
kutumia mionzi maalum ya kutibu maradhi haya na akigundua kuwa ugonjwa
umeenea sehemu mbalimbali za mwili wa mtu anaweza kutumia njia zote kwa
mgonjwa mmoja.
USHAURI
Ni vema kila mtu akawa na kawaida ya kupima afya yake kwani magonjwa
mengi yanapogundulika mapema katika mwili tiba yake huwa ni rahisi kwa
daktari kuutokomeza ugonjwa na pia huwa nafuu kwa mgonjwa kwa kuwa hata
gharama ya tiba huwa ni ndogo.
Ni vizuri pia kwa kila familia kujua kama mna historia ya kuwa na
saratani ya aina yoyote na unapofanyiwa uchunguzi daktari kumfahamisha
jambo hilo kwani kufanya hivyo kutafanya aangalie zaidi.
Ni wazi mtu ambaye familia yake imewahi kutoa mtu aliyeugua saratani ina
nafasi kubwa ya kupata ugonjwa huu kuliko mtu ambaye familia yake
haijawahi kuugua maradhi haya. Uonapo dalili wahi hospitali.

No comments
Post a Comment