Ugonjwa wa uti wa mgongo hutokea iwapo
utando unaofunika ubongo na uti wa mgongo utapatwa na maambukizi.
Ugonjwa wa Uti wa mgongo husababishwa na
nini?
Ugonjwa huu husababishwa na vimelea
mbalimbali vya makundi ya bakteria, virus na hata fungus. Tukivigawanya
visababishi hivi katika makundi haya, tutaona kuwa bakteria wanaosababisha
ugonjwa wa uti wa mgongo ni kama vile; bakteria wajulikanao kama Beta-streptococci,
Hemophilus influenza, Escherichia coli, Listeria monocytogenes, Neisseria
meningitides, Streptococci pneumoniae pamoja na Mycobacteria tuberculosis,
ambao pia ni maarufu kwa kusababisha ugonjwa wa kifua kikuu.
Aidha kutoka kundi la virus, virus
wanaojulikana kwa kusababisha ugonjwa huu wa uti wa mgongo ni pamoja na Herpes
simplex type 2, HIV pamoja na Varicella zoster.
Vimelea vya fungus ambavyo hujulikana kwa
kusababisha ugonjwa wa uti wa mgongo ni pamoja na wale wajulikanao kama Coccoidiodomycosis
pamoja na Cryptococci meningetides.
Dalili za ugonjwa wa uti wa mgongo
Dalili na viashiria vya uti wa mgongo ni
pamoja na
Shingo kukakamaa na kuwa ngumu isivyo
kawaida
Mgonjwa kujihisi homa kali
Maumivu makali ya kichwa
Mgonjwa kupoteza fahamu
Mgonjwa kupatwa na degedege (seizures) na
mwili kukakamaa
Mgonjwa kushindwa kuvumilia mwanga
(photophobia)
Mgonjwa kutoweza kukaa sehemu yenye
makelele (phonophobia)
Kwa watoto, kuvimba utosi
Aidha, wakati wa kumfanyia mgonjwa
uchunguzi, daktari anaweza kuangalia pia viashiria vingine vinavyoonesha kuwepo
kwa ugonjwa wa uti wa mgongo. Ishara hizi ni kama vile
Mgonjwa uhisi maumivu kwenye uti wa mgongo
yanayozuia kukunjua goti wakati anapofanyiwa uchunguzi wa kukunjua goti lake
(pain limits passive extension of the knee). Ishara hii huitwa ishara ya
Kerning au Kerning's sign.
Wakati mwingine mgonjwa anapoelekezwa
kujitahidi kukunja shingo, miguu (yaani paja pamoja na goti) navyo hujikunja
pia (flexion of the neck causes involuntary flexion of the knee and hip).
Ishara hii huitwa ishara ya Brudzinski au Brudzinski’s sign.

Vipimo na uchunguzi
Pamoja na kumchunguza mgonjwa kuhusu kuwepo
kwa dalili na viashiria vya ugonjwa huu wa Uti wa mgongo, daktari pia anaweza
kufanya vipimo vifuatavyo;
Kuchunguza damu ya mgonjwa kwa ajili ya
kuangalia uwepo wa vimelea vinavyosababisha ugonjwa na pia kufahamu ni aina
gani ya vimelea hao. Hali kadhalika, damu inaweza pia kutumika kuotesha vimelea
maabara ili kugundua aina ya vimelea na dawa gani nzuri zinazofaa kwa ajili ya
matibabu (culture and sensitivity).
Kipimo kinachofanyika kwa kuchukua maji ya
uti wa mgongo wa mgonjwa na kuyachunguza maabara ili kutambua uwepo wa vimelea,
aina ya vimelea na dawa zinazofaa kutibu vimelea hao (Lumbar puncture).
Kwa baadhi ya maeneo yenye vifaa kama
CT-scan na MRI, mgonjwa pia huweza kuchunguzwa kwa kutumia vifaa hivi ili
kufahamu uwepo wa ugonjwa, sehemu lilipo na madhara yaliyosababishwa na ugonjwa
huu wa uti wa mgongo. Hata hivyo vipimo hivi haviwezi kutambua aina wala dawa
ya kutibu vimelea vinavyosababisha ugonjwa huo.
Matibabu ya ugonjwa wa Uti wa Mgongo
Kwa wagonjwa waliopoteza fahamu ni vizuri
kuhakikisha wanapumua vizuri, na njia za hewa ziko wazi. Halikadhalika, iwapo
itathibitika kuwa bakteria ndiyo wanaosababisha ugonjwa huu, mgonjwa anaweza
kupewa mojawapo ya dawa hizi za antibiotiki kama cefotaxime au Cefriaxone.
Aidha baadhi ya madaktari hupendelea kuongeza dawa za steroids kama
dexamethasone kama sehemu ya matibabu.
Iwapo itathibitika ugonjwa huu
umesababishwa na virus, dawa kama Acyclovir huweza kutumika. Hali kadhalika,
ikithibitika kuwa vimelea waliosababisha ugonjwa huu ni wa kundi la fungus,
dawa kama Amphotericin B au flucytosine zaweza kutumika. Mgonjwa pia hupewa
Paracetamol kwa ajili ya kushusha homa na kuondoa maumivu ya kichwa.
Madhara yanayoweza kuletwa na ugonjwa wa
uti wa mgongo
Ugonjwa wa uti wa mgongo unaweza
kusababisha
Kuamshwa kwa chembechembe za damu zinazo
sababisha damu kuganda kitaalamu – Disseminated Intravascular Coagulopathy
(DIC).
Kuvuja damu kwa katika tezi za adrenalin na
kupelekea kutokea kwa ugonjwa ambao kitaalamu unaitwa – waterhouse friderichsen
syndrome.
Kwa watoto, ugonjwa huu unaweza kusababisha
mtoto kuwa na kichwa kikubwa - hydrocephalus.

No comments
Post a Comment