Ugonjwa wa kaswende ni ugonjwa wa zinaa unaosababishwa na bakteria
aina ya Treponema pallidum. Ugonjwa huu ni kati ya magonjwa ya zinaa
yanayoongoza kwa kusababisha madhara mengi. Maambukizi ya kaswende
wakati wa ujauzito huleta madhara mengi sana kama vile kujifungua kiumbe
ambacho kimeshakufa, mtoto kuathirika na ugonjwa huu wakati wa
kuzaliwa, mtoto kupata matatizo wakati wa ukuaji wake, degedege na
kuongezeka kwa vifo vya watoto wachanga. Ugonjwa wa kaswende
huathiri zaidi ya mimba milioni moja duniani kote kila mwaka na
kuchangia theluthi mbili ya vifo vya watoto wanaozaliwa wakiwa tayari
wameshakufa katika nchi za maeneo ya chini ya Jangwa la Sahara. Asilimia
30 ya mimba zinazoathiriwa na kaswende huishia watoto kufariki wakati
wa kuzaliwa. Pia asilimia nyingine 30 ya mimba zinazoathiriwa na
kaswende husababisha watoto wanaozaliwa na ugonjwa huu kupata matatizo
ya ukuaji, degedege na kuongezeka vifo vya watoto kwa asilimia 50. Kwa
mfano Taasisi ya kudhibiti Ugonjwa wa Ukimwi nchini Tanzania (Tanzania
National AIDS Control Programme) au NACP katika ripoti yake ya utafiti
uliofanywa chini ya Wizara ya afya na ustawi wa jamii nchini humo
ilitangaza kuwa, maambukizi yote ya kaswende wakati wa ujauzito Tanzania
bara kati ya mwaka 2013 hadi 2015 yaliongezeka kwa wastani wa asilimia
6.7 kwa ujumla, kuanzia mkoani Kilimanjaro ambako maambukizi yalikuwa ya
asilimia 0.4 hadi mkoani Tabora ambako yalikuwa ya asilimia 32.
Magonjwa ya Ukimwi na kaswende mara nyingi huambatana pamoja ambapo
pia ugonjwa wa zinaa wa kaswende huongeza uwezekano wa mtu kupata
Ukimwi.
Je, ugonjwa wa kaswende huambukizwa kwa njia gani? Kama tulivyosema
awali, kaswende husababishwa na bakteria aina ya Treponema pallidum.
Njia za maambukizi za ugonjwa huu ni kama zifuatavyo: 1) Kupitia
kujamiana bila kutumia kinga au ngono zembe na mtu aliyeambukizwa
kaswende. 2) Mama aliyepata ugonjwa wa kaswende wakati wa ujauzito
anaweza kumuambukiza mtoto wake wakati wa ujauzito. 3) Kuambukizwa
kupitia michibuko au mipasuko kwenye ngozi wakati wa kujamiana au wakati
mwingine pale mtu anapogusana na mtu mwenye kaswende ikiwa wote wawili
wana mipasuko kwenye sehemu mbalimbali za ngozi zao. Sio rahisi mtu
kutambua kama ana michibuko au la kwenye ngozi kwani mingine huwa midogo
sana isipokuwa ile inayoweza kuonekana kwa macho, lakini huweza kuwa
njia ya maambukizo. Baada ya kujua visababishi vya ugonjwa huo sasa
tuzibainishe pia dalili zake. Dalili na viashiria vya ugonjwa wa
kaswende hutegemea aina ya ugonjwa wa kaswende wenyewe. Kuna aina tano
za ugonjwa wa kaswende ambazo ni;
Ugonjwa wa kaswende wa awali (Primary syphilis)Ugonjwa wa kaswende
wa pili (Secondary syphillis)Kaswende iliyojificha (Latent
syphilis)Kaswende ya baadaye (Tertiary syphilis)Kaswende ya kurithi
(Congenital syphilis)
Kaswende ya awali (primary syphilis):Dalili ya kwanza ya aina hii ya
kaswende ni kutokea kwa kidonda kidogo cha mviringo (chancre kama
kinavyojulikana kitaalamu) katika sehemu ambayo bakteria wameingilia
na hutokea kati ya siku 10 hadi miezi mitatu (kwa kawaida kuanzia wiki 2
hadi 6) baada ya mtu kupata maambukizi. Kidonda hiki kinaweza kutokea
kwenye sehemu ya haja kubwa, shingo ya kizazi kwa wanawake (cervix),
mdomoni, katika uume, ulimi, vulva, tupu ya mwanamke na sehemu
nyinginezo mwilini. Tezi (lymph nodes) ambazo zipo karibu na sehemu
iliyotokea kidonda hiki kawaida huwa zinavimba baada ya siku 7 hadi 10.
Kidonda hiki hakiambatani na maumivu na kwa kuwa kinaweza kutokea katika
sehemu zilizojificha kama kwenye shingo ya kizazi, sio rahisi mtu
kutambua kama ana aina hii ya kaswende. Kidonda hiki kinaweza kuwepo kwa
muda wa wiki 3 hadi 6 kama mtu hatapata matibabu na hutoweka chenyewe
bila tiba au baada ya kupata tiba. Robo tatu ya wale ambao hawapati tiba
huishia kuingia kwenye kundi la kaswende ya aina ya pili yaani
Secondary syphilis. Aina hii hutokea wiki 4 hadi 10 baada ya mtu kupata
kaswende ya awali. Dalili za aina hii ya kaswende ni: vipele ambavyo
haviwashi katika viganja vya mikono au nyayo za miguu. Vipele hivi pia
vinaweza kutokea mwili mzima au sehemu mbalimbali za mwili. Pia
muathirika huhisi uchovu, kuumwa kichwa, homa, kunyofoka nywele,
vidonda vya koo, kuvimba kwa matezi mwili mzima, maumivu ya mifupa na
kupungua uzito. Kaswende ya aina hii hujitokeza kwa wiki kadhaa na
hutoweka hata bila kupata tiba kwa mtu aliyeathirika. Pia inaweza
kujirudia rudia katika kipindi cha mwaka mmoja hadi miwili na mtu
huingia kwenye kundi la aina ya tatu ya ugonjwa wa kaswende yaani
(latent syphilis) baada ya miaka miwili.
baada ya kuijua kaswende ya aina ya awali na ya
pili, tunasonga mbele na somo letu kwa kuelezea kaswende
iliyojificha (Latent syphilis). Aina hii inajulikana kama kaswende
ambayo inaweza kuthibitika tu kwa kutumia vipimo vya maabara
(serological test) na imegawanyika katika makundi mawili. Kundi la
kwanza ni kaswende iliyojificha ya awali au (Early latent syphilis) kwa
kimombo. Hii ni kaswende ambayo hutokea ndani ya kipindi cha mwaka mmoja
baada ya muathirika kuugua kaswende aina ya pili .Aina hii huwa na
dalili zinazojirudia kama za kaswende ya pili. Kundi la pili ni kaswende
iliyojificha ya kuchelewa au Late latent syphilis. Hii hutokea baada
ya mwaka mmoja wa kuugua kaswende ya aina ya pili (secondary syphilis).
Wakati wa kuugua aina hii ya kaswende, muathirika huwa hana dalili wala
viashiria vyovyote vile na uwezo wake wa kuambukiza mtu mwingine huwa
chini au hawezi kabisa kumuambukiza ugonjwa huu mtu mwingine. Kaswende
ya aina ya nne kama tulivyosema inaitwakaswende ya baadaye (Tertiary
syphilis). Asilimia 30 ya wagonjwa wa kaswende ambao hawakupata tiba
hapo awali huingia kwenye kundi hili na hutokea miaka 15 hadi 30 baada
ya maambukizi ya kaswende. Aina hii inaweza kuathiri viungo kama macho,
ubongo, mishipa ya fahamu, viunganishi vya mifupa au joints, uti wa
mgongo, moyo na mishipa ya damu. Kwa ajili hiyo aina hii ya kaswende ni
yenye madhara makubwa kwani huweza kusababisha upofu, magonjwa ya moyo,
magonjwa ya akili na magonjwa ya mishipa ya fahamu. Huweza kumfanya mtu
kuwa kiziwi na kupungukiwa na kumbukumbu na hata kumsababishia kifo. Pia
aina hii ya kaswende inaweza kuathiri mfumo wa chakula, mfumo wa
kupumua na mfumo wa uzazi. Wapenzi wasikilizaji kaswende ya aina ya
mwisho ni ya kurithi (Congenital syphilis). Aina hii ya kaswende
hutokea wakati wa ujauzito au baada ya mtoto kuzaliwa. Nusu ya wototo
wanaozaliwa huwa hawaonyeshi dalili zozote za ugonjwa huu. Nusu ya
watoto wenye maambukizi ya kaswende hufariki dunia muda mfupi kabla ya
kuzaliwa au baada ya kuzaliwa. Dalili za aina hii ya kaswende kwa mtoto
mchanga zinaweza kutokea baada ya kuzaliwa au wiki 2 hadi miezi 3 baada
ya kuzaliwa. Dalili hizo ni, kutoongezeka uzito au kushindwa kukua,
homa, kukasirika haraka, kutochongoka kwa pua yaani pua linakuwa bapa,
vipele kwenye viganja vya mikono na kwenye nyayo ambavyo huwa ni
vipele vya rangi ya madini ya shaba kwenye uso, viganja vya mikono na
nyayo na vipele kwenye mdomo, sehemu za siri na sehemu ya haja kubwa.
Dalili nyingine ni kutokwa na majimaji puani, kuongezeka ukubwa wa
ini na bandama, ngozi kuwa ya njano, na upungufu wa damu mwilini
(anemia).
dalili za ugonjwa wa kaswende kwa mtoto mkubwa ni,kuathirika meno
(Hutchinson teeth), maumivu ya mifupa, kupata upofu, kupungua uwezo wa
kusikia au mtoto kuwa kiziwi na kuwa na ukungu kwenye mboni za macho
(Clouding of cornea). Dalili nyingine ni kutokwa vidonda vya rangi ya
kijivu kwenye sehemu ya haja kubwa na kwenye tupu ya mwanamke, ngozi
kuwa na mabaka meusi kwenye mdomo, sehemu za siri na sehemu za haja
kubwa, maumivu kwenye mikono na miguu na pia kuvimba jointi za mifupa.
No comments
Post a Comment