Kuna dhana
imejengeka nchini miongoni mwa wanaume kwamba ni wanawake pekee
ndio wenye wajibu wa kuhudhuria kliniki wakati wa ujauzito na baada ya
kujifungua.
Katika miaka ya
karibuni kuna kampeni kubwa ya kuwataka wanaume waongozane na wenza wao
kliniki ili kwa ajili ya kupata ushauri wa kitaalam kuhusu afya ya uzazi.
Makala hii yafafanua zaidi
“KUTOKANA na mila na
desturi, binafsi nilipanga kuzaa watoto watano. Hata hivyo, mume wangu
anaonekana kuwa kinyume na mawazo yangu na amekuwa mara zote akisisitiza kwamba
angependa tuzae watoto watatu tu,” anasema moja ya Mama aliekuja kliniki
nilipomhoji..
Wakati wa mahojiano
haya alikuwa kwenye foleni ya kusubiri huduma ya kliniki katika hospitali moja
hivi. anasema kwamba hadi sasa yeye na mume wake ambaye ni Mkulima wamefanikiwa
kupata watoto wawili ambao wametofautiana kwa miaka miwili.
Anasema kwamba,
tangu alipoolewa amekuwa na mawazo ya kuzaa watoto watano akiamini kwamba
atakuwa amezingatia uzazi wa mpango. Katika familia yake wamezaliwa
watoto 12.
Hata hivyo anasema
kwamba ,anaona kila dalili kuwa ndoto yake ya kuzaa watoto watano huenda
isitimie kutokana na msimamo wa mume wake.
Anabainisha kuwa,
chanzo cha mume wake kuwa na msimamo wa kuzaa watoto wasiozidi watatu ni baada
ya kuhudhuria kliniki na kushauriwa kufanya hivyo.
“Unajua siku hizi
akina mama tunapohudhuria kliniki tunashauriwa kufuatana na wenza wetu.
Nilipomuambia mume wangu alikubali bila kusita,”anasema.
Anaongeza kuwa, tangu
siku ya kwanza alipohudhuria kliniki, mume wake ameonekana kufanyia kazi
ushauri waliopewa na wataalam wa afya ya uzazi ikiwemo kuzaa idadi
ndogo ya watoto watakaoweza kuwatunza.
Anasema kwamba licha
ya kutumia muda mwingi akiwa katika shughuli zake za ukulima, lakini anapokuwa
nyumbani mume wake hufuatana naye kwenda kliniki kwa ajili ya kupima ujauzito
au mtoto na hufundishwa jinsi ya kuzuia maambukizo ya Virusi vya Ukimwi
kutoka mama kwenda kwa mtoto.
Kwa mujibu wa Mama
huyo, hatua hiyo ya mumewe kukubali kuambatana naye kwenda kliniki imeimarisha
ndoa yao kwa sababu kila kitu kuhusu uzazi wanakifanya kwa kushirikiana na kwa
kuzingatia ushauri wa kitaalam.
“Unajua wanaume
wengi wana hulka ya kutopenda kujihusisha kwa karibu na masuala ya afya ya
uzazi.Wanapenda kutuacha sisi wanawake twende kliniki peke yetu.
Inakuwa vigumu kufanyia kazi ushauri wote tunaopewa kwa sababu wengi wetu
hatuna kauli kwa waume zetu,”anasema.
Anafafanua kwamba,
kwa mila na desturi za kabila la wasukuma mwanamke hana mamlaka ya kumpa
maelekezo mumewe, hivyo imekuwa vigumu wanawake kufikisha ushauri
waliopewa kliniki kwa wenza wao.
Hata hivyo anasema
kwamba, kwake hali ni tofauti kwa sababu uamuzi wa mumewe
kukubali kuongozana naye kwenda kliniki kimemsaidia kupata ushauri moja kwa
moja kutoka kwa wataalam na amekuwa akiufanyia kazi.
“Mimi na mume wangu
tunaishi kwa maelewano hasa linapokuja suala la afya ya uzazi. Hakuna mahali
tunabishana kwa sababu kila mtu anajua wajibu wake kwa kuzingatia ushauri
tunaopewa kliniki. Sasa sina simanzi tena kuhusu mapenzi kwa sababu namuamini
mume wangu na yeye ananiamini,”anasisitiza.
Pascal Emmanuel (19)
mkazi wa kijiji cha kisuke wilayani kahama, ambaye amemaliza kidato cha nne
mwaka jana (2012) alionekana ameongozana na msichana mdogo wa rika lake
kwenda katika kliniki ya hospitali ya wilaya hiyo.
Pascal alisema
amefika kliniki kwa ajili ya kumsindikiza mwenza wake mwenye ujauzito
wa miezi sita.
Anasema kwamba,
kimsingi wao si mume na mke kama ambavyo ingeweza kudhaniwa isipokuwa wamekuwa
na uhusiano wa kimapenzi tu huku kila mtu anaishi nyumbani kwa wazazi wake.
pascal anasema
amemaliza kidato cha nne mwaka jana, mwenza wake aitwaye Tatu Mabiti
ameishia darasa la saba, na walipoanza uhusiano wa kimapenzi wakajikuta
wametengeneza ujauzito usiotarajiwa.
Hata hivyo, hali
hiyo haijawa kikwazo kwa pascal kushirikiana na rafiki yake huyo kulea
mimba kwa kuzingatia ushauri wa kitaalam kuhusu afya ya uzazi ikiwemo kinga ya
maambukizi ya VVU kutoka mama kwenda kwa mtoto.
Anasema kuwa, mara
tu alipoambiwa na mwenza wake kwamba wanatakiwa kwenda pamoja kliniki, hakuhisi
ubaya wowote badala yake alikubali, na siku ilipowadia wakaongozana kwenda
kupata ushauri wa kitaalam kuhusu afya ya uzazi.
Anabainisha kwamba ,
licha ya kuambiwa na mwenza wake, kilichomsukuma kwenda kliniki ni taarifa
kuhusu afya ya uzazi ambazo amekuwa akizipata kupitia matangazo mbalimbali ya
redio, televisheni na machapisho.
“Nimekuwa nikisikia
na hata kuona matangazo yanayosema kwamba mwanamke anapopata ujauzito tangu
siku ya kwanza anapaswa kuongozana na mwenza wake kwenda kliniki, kwa hiyo hata
mimi Tatu aliponiambia tuje niliona ni sawa tu,”anasema.
Anaongeza kwamba,
kuongozana na mwenza wake kliniki kumemsaidia kufahamu mambo mengi kuhusu afya
ya uzazi, kwa sababu kuna baadhi ya mambo hayapo kwenye matangazo
lakini ukifika kliniki unayapata.
Aidha anasema
kwamba, kitu kingine alichojifunza ni kwamba mjamzito anapoongozana na mwenza
wake kliniki anahudumiwa kwa haraka zaidi tofauti na wale wanaokwenda
bila wenza wao.
“Kuna kitu hapa
kimenifurahisha kwani ingawa nimekuja na mwenzangu tukiwa tumechelewa
kidogo lakini tulipofika tu mara moja tumepokelewa na kupewa huduma. Hali hii
imenipa somo kwamba wanawake wanaosindikizwa kliniki na wenza wao hawapati adha
ya kukaa kwenye foleni,”anasema.
Mwalimu Mkuu wa
shule ya msingi Kapela wilayani Bukombe Bi Tekla Manyanda anaunga mkono hoja
hiyo kwamba, hata yeye wakati akiwa mjamzito hadi alipojifungua
alijitahidi kumbumbusha Mme kumsindikiza kliniki ili kumuwezesha
kupata huduma kwa haraka nae alifanya hivyo.
Anasema kwamba,
licha ya kupata huduma kwa haraka lakini kuhudhuria kliniki na mme wake kumewasaidia
kujua mbinu nyingi za kupanga uzazi ambazo hazina athari kwao wala kwa watoto.
“Nilipokuwa
namsindikiza mke wangu kliniki nilijifunza mambo mengi sana, kwanza tulipokuwa tunafika
tulihudumiwa kwa haraka bila kujali kama tumewakuta wengine wasio na wenza
wao.Pia imetusaidia kupanga vizuri uzazi tofauti na huko nyuma nilipokuwa
siendi kliniki” alisema Mme wa Mwalimu Mkuu.
Kuna mambo mengine
tulikuwa hatuyazingatii kwa sababu haikuwa rahisi kwa mke wangu kukumbuka na
kuniambia kila kitu alichoelezwa na wataalam,”anasema Mme wa Mwalimu Mkuu.
Neema Dismas (25)
mkazi wa Dodoma anasema kwamba, ingawa inatokea mara chache, lakini
anapoongozana na mumewe kliniki hujisikia fahari sana mbele ya
wanawake wenzake.
“Natamani muda wote
anapokuwa nyumbani tuongozane kwenda kliniki kwa sababu najisikia fahari.Lakini
pia kuna ushauri kuhusu afya ya uzazi tunaopewa pamoja inakuwa
rahisi kuutekeleza,”anasema.
Muuguzi Kiongozi
katika kliniki iliyopo hospitali ya wilaya ya Bukombe Bi Sofia Herman anasema
kwamba siku zote wamekuwa wakiwasisitiza wanawake wajawazito na wenye watoto
kuambatana na wenza wao pindi wanapofika kliniki.
Anasema sababu kubwa
ni kuwezesha wenza wote wawili kupata ushauri wa kitaalam kuhusu afya ya uzazi
ikiwemo uzazi wa mpango na kinga ya maambukizo kutoka kwa mama kwenda kwa
mtoto.
Anasema kwamba,
wakati wa kliniki akina mama hufanyiwa vipimo mbalimbali vikiwemo vya magonjwa
ya zinaa na wale wanaobainika kuambukizwa hupatiwa matibabu bure.
Kwa msingi huo,
anasema kwamba mama anapokuwa ameongozana na mwenza wake inakuwa rahisi kupewa
ushauri wa kitaalam ili kuzuia maambukizo zaidi.
“Kuna baadhi ya kina
mama tunapowapima tunabaini wameambukizwa magonjwa ya zinaa. Kwa sababu
wanakuja peke yao inakuwa vigumu kupata tiba sahihi hata kama
tukimtibu yeye bado akirudi kwa mumewe anaweza kuambukizwa tena,”anasema.
Anatoa mfano kwamba,
hivi karibuni mama mmoja alipimwa na kukutwa ameambukizwa ugonjwa wa kaswende,
wakamshauri akamlete mumewe ili naye apimwe kisha wapatiwe tiba kwa
pamoja.
Hata hivyo anasema
kwamba, mama huyo alipokwenda kumwambia mumewe kuwa anahitajika kliniki aligoma
kwenda huku akidai kuwa hajisikii kuumwa chochote.
Anabainisha kuwa, ndiyo
sababu mara zote wamekuwa wakiwasisitiza akina mama kuongozana na wenza wao ili
kama kuna jambo lolote linalohitaji ufumbuzi wa pamoja iwe rahisi kulifanyia
kazi.
“Mara nyingi wanaume
wanaposhindwa kuja kliniki huwa hawazingatii ushauri tunaowapa wake zao hali
ambayo huchangia sio tu kuzaa watoto bila mpangilio lakini pia maambukizo zaidi
ya magonjwa ya zinaa na hata virusi vya Ukimwi,”anasisitiza.
Anaongeza kwamba,
wanawake ambao hawaongozani na wenza wao kliniki imekuwa vigumu kupata huduma
nzuri katika kipindi cha ujauzito au malezi ya mtoto kwa sababu anayemiliki
uchumi (mume) anakuwa hajui chochote kuhusu afya ya uzazi.
“Hapa wilayani
Bukombe wanaume wengi ndio wanaomiliki uchumi, hivyo wanaposhindwa kuja kliniki
inakuwa vigumu kuwahudumia kikamilifu wake zao katika kipindi cha ujauzito kwa
sababu hawana elimu kuhusu afya ya uzazi, matokeo yake baadhi yao hupoteza
maisha wakati wa kujifungua,”anasema.
Anaongeza kwamba ili
kuhakikisha wanawake wanakwenda kliniki na waume zao, wameweka utaratibu kwamba
anayekwenda na mwenza wake anapewa kipaumbele katika huduma, hata kama
amewakuta wenzake atahudumiwa kwanza.
Anashauri kwamba,
wanaume wajitahidi kuongozana na wenza wao kliniki kwa sababu inasaidia kupatikana
kwa huduma ya uhakika na haraka hospitalini na nyumbani, na kwamba kliniki ni
kwa ajili ya baba, mama na mtoto.
Mratibu wa Huduma ya
Afya ya Uzazi na Mtoto wilayani bukombe anasema kwamba, wanaume wengi katika
wilaya hiyo hawana mwamko wa kuwasindikiza wake zao kliniki.
Wachache ambao
wamepata mwamko wa kuwasindikiza wake zao kliniki anasema, wamekuwa na
mafanikio makubwa katika suala zima la afya ya uzazi hata kumudu kuzaa watoto
wachache wanaoweza kuwatunza na kuzuia mapema maambukizo ya VVU kutoka
mama kwenda kwa mtoto.
Anasema kwamba
wanaume wasiohudhurii kliniki na wake zao wamejikuta wakizaa watoto wengi
wanaoshindwa kuwatunza kwa kuwapa chakula bora na kuwapeleka shule.
“Hapa Bukombe kuna
mtazamo kwamba kuzaa watoto wengi ni fahari, hivyo utakuta wanawake wengi wenye
umri kati ya miaka 25 hadi 40 tayari wamebeba mimba kati ya mara 6 hadi
8, na wengine mara 10 hadi 13,”anasema.
Hata hivyo, anasema
kwamba wengi wao wamejikuta mimba zikitoka kutokana na kushindwa kuzingatia
ushauri wa kitaalam kuhusu afya ya uzazi.
Hivyo Basi ni vizuri
kushirikiana Baba na mama
Kuhudhuria kliniki
ili kupata ushauri wa kia afya kuhusiana na uzazi wa mpango na mambo mengine
yanayoshiana na ushauri wa kina
Kuhusu afya ya mama na mtoto wakati wa
ujauzito.


No comments
Post a Comment