Sehemu ya chini ya kifuko cha uzazi inatwa shingo ya uzazi (cervix). Shingo ya uzazi ina aina mbili za seli kwenye uso wake. Seli hizi zikiathirika huweza kutokea kansa ya shingo ya uzazi.
Virusi aina ya human papillomavirus (HPV) ndivyo vinavyosababisha seli za shingo ya uzazi kubadilika na kuwa kansa. Virusi hivi huambukizwa kwa njia ya kujamiiana. Zipo chanjo za kuzuia kuambukizwa virusi vya HPV. Chanjo hii huwafaa zaidi wasichana ambao hawajaanza tendo la ndoa au wanawake ambao wamethibitika kutokuwa na maambukuzi ya virusi vya HPV.
Wanawake wengi wanapata maambukizi ya HPV, lakini sio wote walioambukizwa hupata kansa ya shingo ya uzazi. Virusi vya HPV huondoka bila matibabu yoyote baada ya takriban miaka miwili, lakini kwa baadhi ya wanawake virusi hivi hubaki kwa muda mrefu. Katika kundi hili la walioambukizwa ambalo virusi hubaki muda mrefu, baadhi yao hupata kansa ya shingo ya uzazi.
Kansa ya shingo ya uzazi hukua kidogokidogo kwa miaka mingi. Hatua zake za awali huwa sio kansa. Hatua hizi zinaweza kuonekana kwa kutumia kipimo cha darubini kinachoitwa colposcopy. Wakati wa kipimo hiki daktari huweza kuchukua sehemu ya shingo ya uzazi yenye dalili za kuathirika (biopsy) na kupeleka maabara kwa vipimo zaidi. Wakati mwingine huweza kuhitajika kuchukua sehemu kubwa zaidi ya shingo ya uzazi (cervical conisation) kwa ajili ya vipimo. Katika hatua za awali za ukuaji wa kansa, cervical conisation huweza kutosha kuondoa sehemu iliyoathirika na mgonjwa kupona kabisa.
Vilevile seli za shingo ya uzazi zinaweza kupimwa kwenye maabara kwa kipimo kinachoitwa Pap Test. Daktari huchukua seli za uso wa shingo ya uzazi na kupeleka maabara kwa vipimo.
Uwepo wa virusi vya HPV unaweza kupimwa kwa kuangalia DNA ya virusi hivyo kwenye kipimo kinachoitwa HPV DNA test.
Katika hatua za awali, kansa ya shingo ya uzazi haina dalili yoyote. Kadri inavyoendelea kukua, huanza kuonyesha dalili za kutokwa na damu wakati wa tendo la ndoa, kutokwa na majimaji ukeni, kutokwa na harufu mbaya ukeni, maumivu ya tumbo, matatizo ya njia ya mkojo na haja kubwa.
Kwa vile virusi vya HPV huambukizwa kwa njia ya kujamiiana, kuepuka uesharati husaidia kupunguza uwezekano wa kupata kansa ya shingo ya uzazi. Wasichana wanaoanza ngono mapema wana uwezekano mkubwa wa kupata kansa ya shingo ya uzazi kuliko wanaochelewa kuanza. Vilevile kuacha kuvuta sigara husaidia kupunguza uwezekano wa kupata kansa ya shingo ya uzazi kwa vile uvutaji sigara unaviwezesha virusi vya HPV kushambulia shingo ya uzazi kwa urahisi.
Ili kuweza kugundua mapema mabadiliko ya shingo ya uzazi yanazoweza kuwa kansa, inashauriwa wanawake wote walioanza kujamiiana wawe wanapimwa kila baada ya muda fulani. Hii ni kwa sababu hatua hizi za awali hazionyeshi dalili yoyote. Vipimo vinavyotumika ni colposcopy, Pap tes, HPV DNA test kama ilivyoelezwa hapo juu.
Iwapo shingo ya uzazi itakutwa na mabadiliko yanayoashiria uwepo wa kansa matibabu huhitajika. Hatua za awali za kansa hutibika kwa njia ya upasuaji. Kutegemeana na hatua iliyopo upasuaji huo unaweza kuhusisha sehemu ya shingo ya uzazi, shingo yote ya uzazi au kifuko cha uzazi na tisho zinazokizunguka. Wagonjwa wengi wanaokutwa kwenye hatua za awali hupona kabisa.
Kwa kansa iliyokutwa kwenye hatua ya kukua mpaka nje ya shingo ya kizazi, matibabu yake hufanyika kwa njia ya upasuaji wa kuondoa kifuko cha uzazi na shingo yake, mionzi, dawa za chemotherapy au mchanganyika wa njia hizi.
Kabla ya kuanza matibabu, mgonjwa hufanyiwa vipimo ili kugundua hatua ya ugonjwa (staging). Baada ya vipimo hivyo, mikakati ya matibabu hupangwa kwa kujadiliana na mgonjwa. Mgonjwa akikubaliana na mikakati inayoshauriwa, matibabu huanza.
Baada ya matibabu, ni vema mgonjwa akawa anafuatiliwa afya yake kila baada ya muda fulani ili kuweza kugundua mapema uwepo wa tatizo lolote na kulipatia matibabu.
Video hizi zinaonyesha jinsi vipimo cha colposcopy na Pap test vinavyofanyika.
1.PAP TEST
2.COLPOSCOPY


No comments