
Ukitembea katika jamii hasa mijini utawasikia watu wengi hasa
wanaume wanapokunywa bia na kula supu wakizungumzia ugonjwa huu wanaoutaja kama
gauti. Unaweza kujiuliza, huu ni ugonjwa gani?
Huu ni ugonjwa unaoathiri viungo vya mwili unaosababishwa na
kuwepo kwa kiasi kikubwa kuliko kawaida cha tindikali aina ya uriki (uric acid)
katika damu.
Ongezeko hilo la uriki husababisha madhara katika viungo vya
mifupa, viungo ni sehemu ya mwili inapokutana, inapoungana mifupa miwili. Kwa
kawaida, gauti inaweza kutokea ghafla au ikawa sugu.
Kwa ile inayotokea ghafla huwa na maumivu makali na mara
nyingi huathiri kiungo kimoja tu wakati gauti sugu inaweza kuathiri kiungo
zaidi ya kimoja na huambatana na hali ya kujirudia ya maumivu na uvimbe kwenye
viungo.
Visababishi vyake
Gauti husababishwa na kuwepo kwa kiwango kikubwa kuliko
kawaida cha tindikali ya uriki katika damu. Hali hii hutokea iwapo mwili wa
mgonjwa unatengeneza uriki nyingi kuliko kawaida au unashindwa kutoa tindikal
ya uriki mwilini kama inavyotakiwa.
Ongezeko hili husababisha mrundikano wa tindikali ya uriki
katika majimaji yanayozunguka viungo yanayoitwa synovial na hatimaye
kutengeneza vijiwe vidogovidogo vya tindikali ya uriki ambavyo husababisha
viungo kuvimba na hatimaye kuathirika.
Vihatarishi
Ingawa chanzo halisi hakieleweki vyema, ugonjwa hutokea
kuwapata baadhi ya watu walio wa familia moja. Wanaume huathiriwa zaidi kuliko
wanawake ingawa wanawake waliokoma kupata hedhi huathiriwa zaidi.
Aidha, unywaji pombe unachangia kwa kiasi kikubwa kuwepo kwa
ugonjwa huu pamoja na matumizi ya baadhi ya dawa kama vile za kutoa maji
mwilini ambazo kwa ujumla husababisha ongezeko la kiwango cha uriki katika
damu.
Vihatarishi vingine ni pamoja na kuwa na ugonjwa wa kisukari,
magonjwa ya figo, unene uliokithiri, upungufu wa damu unasababishwa na seli
mundu (sickle cell) au aina nyingine za upungufu wa damu, pamoja na saratani ya
damu (leukemia).Pia, gauti inaweza kusababishwa na matumizi ya dawa ambazo
utendaji wake kazi huingiliana na utoaji wa tindikali ya uriki mwilini.
Dalili za ugonjwa huo
- Dalili kwa kawaida huhusisha kiungo kimoja au vichache.
Viungo vinavyoathiriwa zaidi ni pamoja na kidole kikubwa cha mguuni, magoti, au
kiwiko cha mguu.
-Wagonjwa huwa na maumivu yanayoanza kwa ghafla, hususan
nyakati za usiku. Mara nyingi mgonjwa hudai anasikia maumivu makali kama kitu
kinachokata, kupwita au mifupa inayosagana.
-Viunganio katika mwili hubadilika na kuwa na joto, kuvimba
na kuwa na nyekundu (hujionyesha zaidi kwa watu wenye ngozi nyeupe). Kwa
kawaida mgonjwa hulalamika maumivu makali ikiwa ataguswa kwenye kiungo chenye
matatizo.
-Shambulio linaweza kudumu kwa siku kadhaa kabla mgonjwa
hajapata nafuu, pia laweza kujirudia mara kwa mara.
-Pia mgonjwa anaweza kujihisi homa. Baadhi ya wagonjwa hupata
gauti sugu ambayo huwaletea madhara sugu katika viungo (chronic arthritis) hali
ambayo husababisha mgonjwa kujihisi maumivu na muda mwingi kushindwa vizuri
kutumia viungo vyake.
Wagonjwa wa muda mrefu huwa pia na vinundu chini ya ngozi
inayozunguka viungo vilivyoathirika. Vinundu hivi ni ishara ya muhimu kwa
madaktari.
Vipimo
-Kiwango cha tindikali ya uriki katika damu. Hata hivyo, si
kila aliye na kiwango kikubwa cha tindikali ya uriki katika damu huwa na gauti.
-Kiwango cha tindikali ya uriki katika mkojo
-Uchunguzi wa maji maji yanayozunguka viungo (synovial fluid)
kuchunguza vijiwe katika viungo.
-X ray ya kiungo kilichoathirika.
-Uchunguzi wa utando unaozunguka jointi (synovial biopsy)
Matibabu
Matibabu hujumuisha matumizi ya dawa, lishe pamoja na
mabadiliko katika tabia na mienendo ya kimaisha ya mgonjwa.
Dawa hutumika mara tu mgonjwa anapopata shambulio la ghafla.
Dawa hizo ni pamoja na:
-Dawa za kutuliza maumivu kama vile codeine, paracetamol
-Dawa za kutuliza mcharuko mwili kama vile ibuprofen
(brufen), indomethacin (indocid), diclofenac.
Pia, ni muhimu mgonjwa kumfahamisha daktari wake iwapo ana
matatizo yasiyoendana na matumizi ya dawa hizi kama vile vidonda vya tumbo au
mzio.
Dawa hizo husaidia kupunguza maumivu, uvimbe, na mcharuko
mwili. Baadhi ya madaktari huchoma sindano dawa ya corticosteroids kwenye
viungio vilivyoathirika ili kupunguza maumivu na uvimbe.
Kwa kawaida, maumivu huondoka saa 12 baada ya kuanza
matibabu, na mgonjwa hupata nafuu kamili baada ya saa 48.
Ili kupunguza kiwango cha tindikali ya uriki katika damu,
mgonjwa hupewa dawa za allopurinol au probenecid kila siku.
Wagonjwa wanaotumia dawa hizi ni wale ambao hupata
mashambulizi ya mara kwa mara ndani ya mwaka au wale ambao hupata mashambulio
makali, wagonjwa waliopata madhara mkubwa kwenye jointi, wagonjwa walio na
vinundu au wagonjwa wenye vijiwe vya uriki katika figo.
Lishe na mabadiliko katika mfumo wa maisha husaidia pia
kuthibiti na kumwepusha mgonjwa na mashambulizi ya mara kwa mara ya gauti.
Ushauri:
-Tuache pombe
-Tupunguze ulaji wa vyakula vyenye viasili vya purine (aina
ya protini) kama vile nyama ya mbuzi, samaki jamii ya sardines na herring,
maini au figo, mkate mtamu, maharage yaliyokaushwa, njegere, baadhi ya uyoga,
spinachi. Dhibiti pia ulaji wa nyama kwa kila mlo.
Jiepushe na matumizi ya vyakula vya mafuta kama vile ice
creams, mayonise au vyakula vya kuokwa. Kula kiasi kikubwa cha wanga. Iwapo
utaamua kupunguza uzito, hakikisha unapunguza kidogo kidogo kwa sababu
upunguzaji wa kasi unaweza kusababisha vijiwe vya uric kujitengeneza katika
figo.

No comments