KWA UFUPI
- Dhana hii potofu imesababisha wazazi wengi kuwapiga marufuku watoto wao kutumia wakidhani ndiyo chanzo kikuu. Leo nitaelezea ugonjwa huo wa mafindofindo ama kwa kitaalamu tonsillitis.
Kumekuwa na uelewa mdogo wa suala la vidonda vya koo maarufu kama mafindofindo katika jamii zetu.
Watu wengi wamekuwa wakiamini ugonjwa huu unasababishwa na
utumiaji wa vitu vya baridi kama kama vile barafu na icecream.
Dhana hii potofu imesababisha wazazi wengi kuwapiga
marufuku watoto wao kutumia wakidhani ndiyo chanzo kikuu. Leo nitaelezea
ugonjwa huo wa mafindofindo ama kwa kitaalamu tonsillitis.
Mafindofindo ni mjibizo wa tezi iitwayo tonsil,
ambayo husaidiana na tezi nyingine katika mwili kupambana na vimelea mbalimbali
vya magonjwa kwa kutengeneza askari mwili.
Tezi hizi ziko mbili na zinapatikana pande zote mbili nyuma
ya koo. Zina rangi ya pinki na mara zinapovimba baada ya maambukizi hubadilika
na kuwa nyekundu.
Mafindofindo ni ugonjwa ambao huambukizwa kwa njia ya hewa,
ambapo vimelea vya magonjwa kama vile bakteria na virusi huenezwa kutoka kwa
mtu mmoja kwenda mwingine kwa njia mbalimbali.
Mojawapo ni kwa kupiga chafya, kukohoa, kugusa zana yenye
vimelea na kugusisha mdomoni au masikioni.
Ugonjwa huu huwapata watoto zaidi ingawa huweza kuathiri
pia watu wa rika nyingine.
Dalili kuu ya ugonjwa huu ni vidonda kooni. Mara nyingi
mgonjwa hulalamika kuwa na vidonda kooni ambavyo huambatana na maumivu makali
wakati wa kumeza chakula.
Dalili nyingine zinazoambatana na vidonda kooni ni uvimbe
wa tezi unaodhihirika mbele ya shingo, homa kali, kichwa kuuma, mafua, harufu
mbaya kinywani, kufifia au kupotea kwa sauti na mwili kuchoka. Vidonda kooni
ambavyo huambatana na dalili nyingine kama vile mafua, kupiga chafya na
kikohozi mara nyingi husababishwa na virusi.
Kwa sababu hiyo, matibabu ya dawa katika hali hiyo si ya
lazima kwa sababu mwili unaweza kupambana katika kuondoa vijidudu hivyo.
Endapo vidonda vya koo havitaambatana na dalili yoyote kama
nilizozitaja, moja kwa moja kinachodhaniwa ni maambukizi ya bakteria.
Njia mbadala za kutibu ugonjwa huu ni pamoja na kupumzika,
kusukutua kinywa kwa kutumia maji vuguvugu yenye chumvi na kunywa maji mengi.
Dawa za maumivu na homa hutolewa na wakati mwingine dawa za
vijaviuasumu (antibiotics) huweza kutumika iwapo maambukizi ni ya bakteria.
Endapo ugonjwa hautapatiwa tiba ya haraka, madhara
mbalimbali huweza kujitokeza kama vile homa yarheumatic, magonjwa ya
sikio, figo, tezi nyingine pia katika mwili zaweza kuathiriwa pia kwa
kutengeneza usaha.
Mwendelezo wa maambukizi ya tezi hizi za koo, huweza
kusababisha mafindofindo sugu. Hii ni kutokana na kuendelea kuzaliana kwa
bakteria ambao hutengeneza vifuko vidogo kwenye tezi hizo.
Ndani ya vifuko hivi hutengenezwa mawe madogo yaliyo na
mchanganyiko wa salfa ambayo huleta harufu mbaya ya kinywa. Mara nyingi
mafindofindo sugu hutibiwa kwa njia ya upasuaji. Hii huamriwa na daktari endapo
maambukizi hayo yatakuwa yameendelea kumsumbua mgonjwa kwa kipindi kirefu.
Upasuaji utamsaidia mgonjwa kuepuka madhara kwenye mifumo mingine.
Ili kuepuka kupata maambukizi katika mfumo wa hewa ni vyema
kuzingatia usafi wa mwili na mikono.
Epuka sehemu ambazo utakaa muda mrefu ambazo
zinavihatarishi kama vile msongamano wa watu na vumbi


No comments