Japo
wengi wetu tumekuwa na mitazamo kwamba, visigino kupasuka ni ishara ya
mtu kutojali usafi wa miguu yake, ila mpenzi msomaji leo napenda
kukushirikisha mambo kadhaa kuhusu mtu kupasuka visigino.
Kwa kawaida, ngozi zetu huwa zina unyevunyevu ambao huiwezesha ngozi ivutike au kutanuka pamoja na kusinyaa bila ya kutokea madhara yoyote kama vile kuchanika. Pamoja na ngozi kugawanyika katika sehemu tatu ( sehemu ya nje – Epidermis, sehemu ya kati – Dermis na sehemu ya ndani – Endodermis), ni sehemu ya nje, epidermis, ambayo ipo karibu na unaweza kuigusa au inaweza kuathirika na ukaiona kirahisi, na hii ni kwa sababu inagusana moja kwa moja na mazingira yetu. Gaga huanza hutokea katika sehemu hii ya ngozi, Epidermis.
Miongoni mwa sababu zinazoweza kumfanya mtu apasuke visigino ni pamoja na:
Ngozi
kuwa kavu sana, hii ni sehemu ya nje ya ngozi ambayo inawezekana mtu kwa
asili yake akawa na ngozi kavu na hivyo kuifanya ishindwe kustahimili
kutanuka au kusinyaa na hivyo kupelekea ipasuke.
Kuiweka
miguu katika maji kwa muda mrefu na baadae kutoipaka mafuta ya
kulainisha ngozi, hii husababisha ile asili ya ngozi pamoja na mafuta
katika ngozi yapotee na kuiacha ngozi ikiwa kavu sana.
Kuwa na
uzito mkubwa, hii husababisha presha kubwa iwe katika miguu unapokanyaga
na endapo ngozi yako haitokuwa na uimara wa kutosha itasababisha
visigino vipasuke.
Upungufu wa virutubisho mwilini, mfano madini ya Zinc, vitamini E pamoja na mafuta, omega 3. Hii husababisha ngozi kupoteza uimara wake na kuifanya ipasuke kirahisi.
Kuvaa
viatu ambavyo nyuma vipo wazi, back-opened shoes or sandals, hii
huulazimisha mguu au upande wa kisigino katika mguu utanuke zaidi na
hivyo kuuweka mguu hatarini kupasuka.
Baadhi ya magonjwa kama vile kisukari na magonjwa ya homoni (thyroid diseases). Hii huathiri afya ya ngozi.
Umri
mkubwa, kwa kawaida mtu anapokuwa na umri mkubwa sana, hata utendaji
kazi wa mifumo mbalimbali katika mwili wake hupungua kiufanisi, hivyo
hata kinga ya mwili pamoja na afya ya ngozi pia hupungua.
Mtu kutozingatia usafi wa miguu yake kwa kiwango kinacho stahili.
Moja ya
madhara yanayoweza kutokea kwa mtu kupasuka visigino ni kupata
maambukizi ya magonjwa, infection. Hii ni endapo miguu itachanika
kiwango cha kufikia ngazi ya kati ya ngozi, dermis, kiasi cha kupelekea
damu zianze kutoka sambamba na maumivu makali. Kupitia hiyo mipasuko mtu
anaweza kupata maambukizi ya magonjwa.
Mambo yanayoweza kufanyika ili kuzuia au kutibu tatizo la kupasuka visigino ni pamoja na:
Kuzingatia ipasavyo usafi wa miguu na mwili kwa ujumla.
Kuepuka kutembea katika sehemu zisizo sawa, rough surfaces, bila kuvaa viatu, hii itaepusha miguu kuchanika.
Kwa
miguu iliyopasuka tayari, ifanyie usafi miguu yako na kisha tumia mafuta
ya mzaituni kupakaa mipasuko, vaa soksi na viatu vya kufunika ili miguu
iendelee kuwa na unyevu, wakati wa usiku pia fanya hivyo huku ukilala
miguu imevalishwa soksi baada ya kuipakaa mafuta.
Ambatanisha
vitu vifuatavyo katika mlo wako, vyakula venye madini ya calcium, zinc
na iron. ( Maziwa, mboga za majani, mafuta ya mimea, nyama, maharage
pamoja na samaki wa maji baridi).
Kuepuka kusimama kwa muda mrefu pamoja na kutoiweka miguu katika maji kwa kipindi kirefu. Kama unafanya zoezi la ufuaji, jitahidi kuilinda miguu yako isiwe katika sabuni kwani sabuni nyingi za kufulia huvunjavunja mafuta yaliyo katika ngozi na kuiacha ikiwa kavu sana na kuifanya ipasuke.
Jitahidi
walau mara moja kwa wiki, kuiweka miguu yako katika maji ya vuguvugu,
hii husaidia kuongeza mzunguko wa damu katika miguu na hivyo kuendelea
kuimarisha afya ya ngozi yako.
Mpenzi msomaji, japo kwa uchache natumai utakuwa umepata jambo kupitia somo hili,
Kumbuka kuwa mambo yote yanayoandikwa au kujadiliwa ndani ya blog hii, ni yale yote yanayohusiana na Afya.


No comments