
MATATIZO YA KUKOSA USINGIZI yamekuwapo tangu zamani.
Leo
mamilioni ya watu hawapati usingizi wa kutosha. Kulingana na mtaalamu
wa usingizi kutoka Brazili Rubens Reimão, inakadiriwa kwamba asilimia 35
ya watu ulimwenguni wana ugonjwa wa kukosa usingizi.* Dakt. David
Rapoport wa Kituo cha Matatizo ya Usingizi katika Chuo Kikuu cha New
York alisema kwamba kukosa usingizi ni “mojawapo ya magonjwa mabaya sana
mwanzoni mwa karne ya 21.”
Jambo
baya zaidi ni kwamba watu wenye ugonjwa huo hawajui kuwa ni wagonjwa.
Kulingana na watafiti wa Chuo Kikuu cha Federal huko São Paulo, Brazili,
asilimia 3 tu ya wagonjwa ndio hupimwa ifaavyo. Wengi huona kukosa
usingizi kuwa jambo la kawaida na hivyo wao husinzia-sinzia na kusumbuka
mchana kutwa.
Inapokuwa Vigumu Kupata Usingizi
Kugeuka-geuka
kitandani kwa saa nyingi, ukiwa macho, huku watu wengine wote wakiwa
wamelala fofofo ni jambo lisilopendeza kamwe. Hata hivyo, ni kawaida
kukosa usingizi mara kwa mara kwa sababu ya mikazo na hekaheka za
maisha. Lakini mtu anapokosa usingizi kwa muda mrefu huenda akawa na
matatizo ya kihisia-moyo au ya kitiba, na ni muhimu amwone daktari.
Je, una ugonjwa wa kukosa usingizi?
Ikiwa
baada ya kujibu maswali hayo, unagundua kwamba una tatizo la kukosa
usingizi, usikate tamaa. Kutambua kwamba una tatizo hilo ni hatua muhimu
ya kulitatua. Mtaalamu wa neva Mbrazili Geraldo Rizzo, alisema asilimia
90 ya watu wenye ugonjwa huo wanaweza kutibiwa na kupona.
Hata hivyo, ili upate matibabu yafaayo, ni muhimu kujua hasa ni nini kinachosababisha ugonjwa huo. Uchunguzi wa kitiba unaoitwa polysomnogramumetumiwa kupima na kutibu magonjwa mengi ya kukosa usingizi.
Mojawapo
ya visababishi vya kawaida vya kukosa usingizi kwa muda mrefu miongoni
mwa watu wazima ni kukoroma. Iwapo umewahi kulala karibu na mtu
anayekoroma, unajua kwamba jambo hilo huudhi sana. Kukoroma kunaonyesha
kwamba mtu ana tatizo la kuziba koo, na hivyo mapafu yake hayapati hewa
ya kutosha kwa muda fulani.
Hatua
za kwanza za kutibu ugonjwa huo zinatia ndani kupunguza uzito, kuepuka
pombe, na kutotumia dawa za kulegeza misuli. Wataalamu wa tiba wanaweza
pia kudokeza mtu atumie dawa fulani au vifaa vinavyotiwa mdomoni au mashine inayoingiza pumzi mapafuni.*
Hali
inapokuwa mbaya zaidi, huenda mgonjwa akahitaji kufanyiwa upasuaji wa
kurekebisha koo, taya, ulimi, au pua ili hewa iingie na kutoka kwa
urahisi anapopumua.
Pia
watoto wanaweza kupata ugonjwa wa kukosa usingizi. Dalili za kukosa
usingizi zaweza kuonekana akiwa shuleni, kwa mfano, kuanguka mitihani,
kuudhika upesi, na kukosa utulivu. Huenda ikafikiriwa kimakosa kwamba
yeye ni machachari.
Watoto
fulani hupambana na usingizi kwa kuimba, kuzungumza, kusikiliza hadithi
au kufanya jambo lolote ili wasilale. Huenda wakatumia ujanja huo ili
wakae na wazazi wao. Hata hivyo, nyakati nyingine, huenda mtoto akaogopa
kulala kwa sababu ya kuota ndoto mbaya zinazosababishwa na sinema zenye
kutisha, matangazo yenye jeuri, au ugomvi nyumbani. Wazazi wanaweza
kuzuia matatizo hayo kwa kudumisha amani na upendo nyumbani. Bila shaka,
matatizo yakizidi wanapaswa kumwona daktari. Ni dhahiri kwamba, watoto
wanahitaji usingizi wa kutosha sawa na watu wazima.
Jinsi ya Kupata Usingizi wa Kutosha
Kwa
karne nyingi imejulikana kwamba usingizi wa kutosha hauji kimuujiza.
Kulala vizuri hutegemea mambo kadhaa mbali na kuepuka wasiwasi na
mikazo.
Kupata
usingizi wa kutosha usiku ni muhimu maishani. Hutia ndani kufanya
mazoezi kwa ukawaida wakati ufaao kila siku. Kufanya mazoezi asubuhi au
jioni kwaweza kumsaidia mtu apate usingizi wakati wa kulala. Lakini
kufanya mazoezi kabla ya kulala kwaweza kuvuruga usingizi.
Kutazama
sinema zenye kusisimua au kusoma vitabu vyenye hadithi motomoto pia
kwaweza kutufanya tusilale. Ni heri kusoma kitabu kinacho starehesha,
kusikiliza muziki wenye kutuliza au kuoga kwa maji moto.
Wataalamu
wanasema kwamba unaweza kuzoeza ubongo wako kutambua wakati wa kulala
kwa kujilaza kitandani wakati tu unapotaka kulala. Watu wanaokula,
kusoma, kufanya kazi, kutazama televisheni, au kucheza michezo ya video
kitandani huenda wasipate usingizi kwa urahisi.
Kuutayarisha
mwili kwa ajili ya usingizi pia hutia ndani kuwa mwangalifu kuhusu
unachokula na kunywa. Ingawa kunywa pombe kunaweza kumfanya mtu asinzie,
kunaweza kuharibu usingizi. Kahawa, chai, koko, chokoleti, na vinywaji
vilivyo na kola vyapasa kuepukwa usiku kwa sababu vinausisimua mwili.
Kwa upande mwingine, kula maembe, viazi vitamu, ndizi, persimmon, machipukizi ya mitende, wali, machipukizi ya maharagwe, au njugu huchochea homoni iitwayo serotonin na kwaweza kuleta usingizi.
Onyo: Kula chakula kingi usiku sana kunaweza kuharibu usingizi kama tu kulala ukiwa na njaa.
Ni
muhimu pia kudumisha hali zinazofaa mahali tunapolala. Hali-joto
inayofaa, chumba chenye giza kisicho na kelele, godoro na pilo zenye
kustarehesha huchangia usingizi mnono.
Ama
kweli, huenda ukashindwa kuamka asubuhi kwa sababu ya starehe hizo
zote. Lakini kumbuka kwamba kulala muda mrefu isivyo lazima, hata kwenye
mwisho-juma,
kwaweza kuvuruga usingizi wako na kukuzuia kulala siku ifuatayo:
Kwa
kweli, hungependa kudhuru kimakusudi kiungo chochote mwilini mwako.
Usingizi ni muhimu, ni sehemu ya maisha ambayo haipasi kupuuzwa. Ama
kweli, sisi hulala thuluthi moja ya muda wote wa maisha yetu.
Je, unaweza kuboresha usingizi wako? Anza leo!
VISABABISHI VIKUU VYA UGONJWA WA KUKOSA USINGIZI
▪ KITIBA: ugonjwa wa Alzheimer; kuziba
koo; miguu isiyotulia; ugonjwa wa kutetemeka; kuamka-amka usiku kwa
sababu ya kushtuka-shtuka; ugonjwa wa pumu; magonjwa ya moyo na tumbo
▪ KIAKILI: kushuka moyo, wasiwasi, hofu ya ghafula, misukumo ya kupita kiasi, mfadhaiko unaosababishwa na tukio lenye kutisha
▪ KIMAZINGIRA: mwangaza, kelele, joto, baridi, godoro lisilostarehesha, kulala na mwenzi asiyetulia kitandani.
▪ SABABU NYINGINEZO: pombe na dawa za kulevya, athari za dawa fulani
KUPIMA MAGONJWA YA KUKOSA USINGIZI
Polysomnogram
ni uchunguzi mbalimbali unaofanywa huku mgonjwa akiwa amelala katika
hali za kawaida. Vifuatavyo ni baadhi ya vipimo muhimu katika uchunguzi
huo.
▪ Electroencephalogram—Hupima utendaji wa ubongo na hutumiwa kupanga na kupima vipindi mbalimbali vya usingizi.
▪ Electrooculogram—Hurekodi misogeo ya macho wakati yanaposogea haraka-haraka usingizini.
▪ Electromyogram—Hutumiwa kuchunguza ulegevu wa misuli ya miguu na kidevu wakati macho yanaposogea haraka-haraka usingizini.
▪ Electrocardiogram—Hutumiwa kupima mpigo wa moyo usiku kucha.
▪ Hali ya kupumua na misogeo ya mwili—hewa inayopitia katika pua na mdomo hupimwa pamoja na kusogea kwa tumbo na kifua.
▪ Kiasi cha oksijeni katika damu—hupimwa kwa kifaa kinachoitwa oximeter kinachounganishwa na kidole cha mgonjwa




No comments